Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo jijini Arusha leo.
Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha,Dk Eliamani Sedoyeka akizungumza katika uzinduzi huo jijini Arusha leo
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ,Nape Nnauye akizindua programu hiyo hiyo jijini Arusha leo.
………………………………
Julieth Laizer ,Arusha .
Arusha .Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amezindua programu ya Shahada ya Media Anuwai na Mawasiliano kwa Umma katika chuo cha uhasibu Arusha-Kampasi ya Arusha .
Akizindua kozi hiyo leo julai 20 ,2023 jijini Arusha Nape amesema kuwa,kitendo cha kuzinduliwa kwa programu mpya chuoni hapo ni jambo kubwa sana kwa maslahi ya nchi na linapaswa kuigwa na vyuo vingine ili kuweza kupata wataalamu wengi zaidi waliobobea katika fani hiyo.
Nape amesema kuwa,kuwepo kwa programu hiyo katika chuo hicho kutasaidia kupata wataalamu bora na wa kipekee waliobobea na kuondokana na changamoto ya kuwa na wanataaluma katika fani hiyo ambao hawajabobea katika maswala ya habari.
“Nakipongeza sana chuo hiki kwani kimeamua kuanzisha programu hii kulingana na uhitaji wa soko ulivyo hivi sasa kwani hivi sasa soko linategemea sana teknolojia ya mawasiliano kwani tunakabiliwa sana na mabadiliko makubwa yanayohitaji wataalamu waliobobea katika fani ya maswala hayo “amesema Waziri Nape.
Aidha amesema kuwa, kitendo cha kuanzishwa kwa programu hiyo mpya chuoni hapo itasaidia sana uchumi wa nchi kukua kwa kusambaza taarifa sahihi kwa ukuaji wa nchi kiuchumi.
Aidha Waziri Nape aliuomba uongozi wa chuo hicho kufikiria namna ya kuanzisha kozi fupifupi ambazo zitawawezesha wale ambao walishapitia kozi zingine kuweza kujifunza zaidi huku wakiahidi kutoa ushirikiano kwa chuo hicho ili kuhakikisha jambo hilo linafika mbali zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha ,Prof Eliamani Sedoyeka amesema kuwa,chuo hicho katika mwaka wa masomo 2023/2024 wanatarajia kuanzisha kozi mpya tano ambapo kati ya hizo kozi za shahada ni nne na moja ya shahada ya Uzamili.
Amesema kuwa ,kuanzishwa kwa kozi hizo kunafanya IAA kuwa na jumla ya kozi 71 ambapo kati ya hizo kozi 16 ni ngazi ya cheti,kozi 17 za stashahada ,kozi 24 za shahada na kwa upande wa shahada ya Uzamili ni kozi 14.
“Moja ya mikakati ya chuo chetu ni kuongeza kozi zinazoendana na mahitaji ya soko letu kwa sasa nchini, kwani chuo bado kinaendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kujua mahitaji ya Watanzania ili kiweze kuanzisha kozi mbalimbali zinazokidhi mahitaji yao katika kuondoa aidha wanayoipata watanzania kwenda kutafuta hizo kozi nje ya nchi kwa gharama kubwa”amesema Prof Sedoyeka.
Profesa ameongeza kuwa, katika zama hizi za kidigitali na mabadiliko ya kasi katika teknolojia ,Tasnia ya habari na mawasiliano inakabiliwa na changamo mpya na fursa za pekee ndio maana wameona umuhimu wa kuwa na programu hiyo ,ambapo chuo hicho kimekuwa cha kwanza nchini kuanzisha kozi hiyo ikiwa imeunganisha pamoja media anuwai na mawasiliano kwa umma.
Naye Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo cha Uhasibu Arusha,Dk Mwamini Tulli amesema kuwa,ubunifu uliofanywa na chuo hicho ni jambo kubwa na linapaswa kuigwa na vyuo vingine kwani kuanzishwa kwa kozi hiyo ni kuona umuhimu wa kutoa fursa kwa vijana wa kitanzania kusoma shahada hiyo muhimu katika tasnia ya habari na mawasiliano.
Ameongeza kuwa, uzinduzi wa shahada hiyo unadhihirisha jinsi chuo hicho kinavyowekeza katika kutoa elimu bora na kukidhi mahitaji ya wakati ,ambapo ametoa wito kwa wazazi pamoja na walezi kukitumia vizuri chuo hicho kuhakikisha wanapeleka watoto wao kujifunza zaidi.