Na Mathias Canal, Rombo-Kilimanjaro
Mbunge wa Viti maalumu Mhe Ummy Nderiananga ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) ameunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuviwezesha vikundi vya wanawake kutumia nishati safi ya kupikia kwa kutoa Mitungi ya gesi.
Naibu Waziri Mhe Nderiananga ametoa mitungi hiyo wakati akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro huku akisisitiza umuhimu wa nishati hiyo mbadala.
Mhe Nderiananga amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuhakikisha inapunguza matumizi ya kuni, mkaa na mabaki ya mazao ili kulinda afya za wananchi.
Amesema kuwa licha ya athari za kimazingira zinazotokana na ukataji wa miti unaofanywa na Wananchi Matumizi ya nishati chafu yamekuwa na athari zaidi za kiafya.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo programu ya kumtua mama ndoo kichwani lakini akasema wakina mama wanapata shida wao ndio wapishi sasa ni wakati wa kuwatua kuni kichwani kwa kuwasaidia kupata nishati ya gesi na mimi nimekuja kutekeleza adhma yake ya kumtua mama kuni kichwani” Amekaririwa Mhe Ummy
Pia amesema kuwa dhumuni la Mheshimiwa Rais ni kuona namna ya kuwakomboa wanawake hususani vijijini hutumia saa nne hadi tano kutafuta kuni, hivyo wanakutana na majanga mbalimbali ikiwemo kung’atwa na wanyama wakali na kutumia muda mwingi kutafuta kuni porini.
Aidha, ameahidi kuendelea na programu hiyo wakinamama kuwatua kuni kichwani na kusaidia kulinda mazingira.