Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nzugilo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao katika Kijiji hicho, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi za kijiji kwa kijiji kwa ajili ya kuzungumza na wanachi wa Jimbo hilo la Kibakwe analoliongoza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akipokea taarifa ya Kijiji cha Idodoma kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Bw. Hashimu Kolezani wakati wa mkutano wake wa hadhara na wananchi wa Kijiji hicho uliolenga kuelezea changamoto mbalimbali za kijiji ikiwemo namna ya kuwabaini walengwa wa TASAF, Ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi za kijiji kwa kijiji kwa ajili ya kuzungumza na wanachi wa Jimbo hilo la Kibakwe analoliongoza.
Sehemu ya wananchi wa Kijiji cha Nzugilo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza nao wakati ziara yake ya kikazi katika kijiji hicho, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuwasikiliza wananchi ambao ni walengwa halisi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi za kijiji kwa kijiji kwa ajili ya kuzungumza na wanachi wa Jimbo hilo la Kibakwe analoliongoza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambaye pia ni Diwani wa Mpwapwa Mjini, Mhe. George Fuime akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Nzugilo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma
Na. Lusungu Helela-Kibakwe
Wananchi wa Kata ya Malolo iliyopo Jimbo la Kibakwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wamepaza sauti zao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakimuomba asaidie kubadili mchakato wa kuwapata walengwa halisi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) huku wakisisitiza kuwa utaratibu unaotumika kwa sasa umegubikwa na sintofahamu.
Aidha, Wananchi hao wamewataka walengwa wa Mpango huo ambao tayari wameimarika kiuchumi kuwa na utu kwa kujiondoa na kuwapisha wengine wanaostahili kuingizwa kwenye Mpango.
Hayo yamesemwa na Wananchi mbalimbali kwa nyakati tofauti kupitia mikutano ya hadhara ya Waziri huyo anayoendelea kuifanya katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo wananchi hao wameomba ubainishaji huo wa walengwa ufanyike kwa uwazi ikiwezekano kupitia mikutano ya hadhara ili waweze kuwapata walengwa halisi.
Wamefafanua kuwa licha ya TASAF kuwashirikisha viongozi wa vijiji husika katika kuwabaini Walenga halisi lakini bado hawaridhishwi na jinsi mchakato unavyoendeshwa kwani kuwekuwa na usiri wa hali ya juu.
Wamesema kuwa mchakato huo katika ngazi za vijiji haufanyiki vizuri hivyo kupelekea wale ambao sio maskini halisi kuwa wanufaika ilhali wale maskini halisi wakiendelea kutaabika.
Malalamiko hayo ya wananchi yalitokana na maswali ya Mhe. Simbachawene ya kutaka kuwatambua walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kata hiyo ya Malolo na namna walivyopatikana ili kujiridhisha na minongóno aliyoisikia juu ya upatikanaji wa walengwa hao.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Simbachawene amesema tayari ameshatoa maelekezo kwa Menejimenti ya TASAF Makao Makuu kuangalia namna bora ya kuwapata walengwa halisi wa Mpango.
Ameongeza kuwa TASAF msingi wake ni mpango shirikishi wa kuondoa umasikini uliokithiri kwa wananchi, hivyo ni lazima kutafuta njia sahihi ili kutimiza azma ya kuanzishwa kwake.