Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri (kulia) wakikaguzi ujenzi wa madarasa yanayojengwa katika Shule ya Sekondari Msalato wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo katika shule hiyo.
Katika picha ni darasa 1 kati ya 7 yaliyojengwa katika Shule ya Sekondari Msalato kupitia fedha kutoka Serikali Kuu hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 85 na wako katika hatua za ukamilishaji. Kiasi cha shilingi milioni 688 zimetumika katika kukamilisha ujenzi wa mabweni manne, vyumba saba vya madarasa na matundu 10 ya vyoo katika shuleni hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wanafunzi pamoja pamoja na Walimu wa Shule ya Sekondari Msalato mara baada ya ziara yake katika Shule hiyo ya Ukaguzi wa Ujenzi wa Mabweni 4, vyumba 7 vya Madarasa na matundu ya vyoo 10 unaoendelea katika shule hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na mwanafunzi wa Kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Msalato Bi. Lucia Izengo Makeremo wakati ziara yake ya kukagua ujenzi wa madarasa na miundombinu ya mabweni katika shule hiyo. Senyamule pia aliwapongeza walimu na wanafunzi hao kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita. Wengine katika picha kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri na Mkuu wa Shule ya Msalato Mwl. Mwasiti Msokola.
Na.Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Shule ya vipaji maalumu ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato Mkoani Dodoma kufuatia matokeo mazuri ya kidato cha Sita kwa kupata ufaulu wa alama ya daraja la kwanza 139 na 6 kwa daraja la pili.
Pongezi hizo amezitoa leo tarehe 17,7.2023 wakati ya ziara yake ya kikazi ya kukagua hatua ya ujenzi wa mabweni manne, vyumba saba vya madarasa na matundu 10 ya vyoo katika shule hiyo na Shule ya Sekondari Bihawana ambapo ujenzi wa matundu sita ya vyoo, bweni moja na vyumba vinne vya madarasa chini ya fedha kutoka serikali kuu. Katika shule ya Sekondari Msalato awamu ya kwanza ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 428 na awamu ya pili shilingi milioni 260 ikiwa ni nyongeza kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliopangwa kuhitajika mabweni mawili ya ziada na Sekondari ya Bihawana shilingi milioni 227.2
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza walimu na wanafunzi kwa kuufaharisha Mkoa wetu wa Dodoma, tunatamani kila mtu anaefanya kazi Mkoani hapa aifaharishe kwa nafasi yake kama hivi mlivyo fanya ninyi hongereni sana mmetupa heshima kubwa sana na nimategemeo yetu kuwa mtaendelea kufanya vizuri zaidi”, ameeleza Mhe.Senyamule
Awali, Mhe.Senyamule amekagua ujenzi unaoendelea shuleni hapo na kuwaasa wakandarasi wanaosimamia miradi kuhakikisha wanaongeza kasi ya umaliziaji wa miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuzingatia muda uliobaki ili wanafunzi wa kidato cha tano wanapoingia waweze kutumia miundombinu hiyo, ikiwa imekamilika kwa ubora unaotakiwa.
“Lazima siku zilizobaki mjitahidi kuongeza kasi na kuongeza ubunifu ili kuendana na wakati uliobaki kwa kuzingatia ubora unaotakiwa, ongezeni idadi ya mafundi na ongezeni masaa ya kufanya kazi, hapa inahitajika speed and accuracy bahati nzuri hapa umeme upo tumieni nafasi hii kukamilisha kazi hii” amesisitiza Mhe.Senyamule
Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Bihawana Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Liberatus Nkilema amesema ujenzi katika Shule hiyo uko katika hatua za ukamilishaji na mkakati uliopo ni kukamilisha mradi huo wa ujenzi ifikapo tarehe 30/07/2023.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri amesisitiza umakini katika hatua ya umaliziaji wa mradi ili kuwa na majengo bora yatakayodumu kwa muda mrefu. Shekimweri pia amesema Mkoa wa Dodoma umefanya vizuri sana katika matokeo ya kidato cha sita ambapo katika Shule kumi bora kitaifa, Dodoma ziko shule 5 na katika Wilaya ziko Shule 10.
Nae,Mwanafunzi Gloria Frank Shirima Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Msalato akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake amemshukuru Mhe,Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha sekta mbalimbali hususani sekta ya elimu ameahidi kuongeza bidii kwenye masomo ili kuongeza ufaulu wa shule na kutendea haki bidii za Mhe. rais.
Bihawana na Msalato ni miongoni mwa Shule za Sekondari nchini zilizopokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha Tano wanaotaraijiwa kuripoti kuanzia tarehe 14 Agosti 2023. Bihawana Sekondari ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 227.2 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 6 ya vyoo, ujenzi wa Bweni 1 na vitanda 40, vyumba vinne vya madarasa vikiwa na jumla ya viti na meza 160.