Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Tume ya Tehama Tanzania (ICTC), Dkt. Mwasaga Nkundwe amesema kesho kampuni kubwa 15 za Tehama kutoka Misri zitakutanishwa na kampuni za hapa nchini ili kubadilisha uzoefu utakaokuza sekta hiyo.
Dkt. Nkundwe ameyasema hayo Julai 18, 2023 kwenye maonyesho ya biashara baina ya Wafanyabiashara wa Zanzibar na Misri mjini yaliyofanyika visiwani humo.
“Tume ya Tehama inaleta kampuni kubwa za Tehama kutoka Misri ili yaweze kukutana na kampuni za Tanzania kujenga daraja la pamoja katika Tehama na kukuza sekta hiyo ambapo kampuni hizo zitakutana kesho Julai 19, 2023 jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni,” amesema
Amesema miongoni mwa mambo yanayolengwa kujadiliwa ni kutatua changamoto ya sekta ya utalii kwakuwa Misri wamepiga hatua kubwa katika eneo hilo.
“Hizi kampuni ni kubwa zinateknolojia mbalimbali na eneo mojawapo amba ni la msingi kwetu sisi ni ubunifu waliofanya kutatua sekta ya utalii na eneo jingine ni kusaidia vyuo vya Tanzania ambavyo vina ubunifu utakaosaidia kutengeneza magari yanayotumia umeme ambapo tayari kuna watu wameshaonyesha uwezo wao,”amesema.
Amesema “Sasa hawa wapo tayari kushirikiana na hivyo vyuo kujenga hayo magari ambayo yatakuwa yanaendeshwa bila mtu kwasababu teknolojia wanayo na vilevile kusambaza betri ambazo hazitumii umeme mkubwa.”