Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akiwa katika mkutano na ujumbe wa Taasisi ya kifedha ya Uingereza (Investment Director Infrastructure), iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Simon Cheung (kushoto), mkutano ulifanyika Ofisi za Hazina, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Taasisi hiyo, Bw. Ope Onibokun.
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mwenyekiti wa Taasisi ya kifedha ya uwekezaji ya Uingereza, Bw. Simon Cheung (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Taasisi hiyo, Bw. Ope Onibokun (wa pili kulia), Mkuu wa masuala ya Uwekezaji kwenye Miundombinu, Bw. Tabish Shariff (kushoto) na kulia ni Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dar es Salaam)
Na. Scola Malinga, WFM, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameikaribisha Taasisi ya kifedha ya Uingereza inayojihusisha na uwekezaji (British International Investment) kufanya uwekezaji nchini katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo ya Nishati.
Dkt. Nchemba, ametoa wito huo alipokutana na kufanya majadiliano na ujumbe wa British International Investment, katika Ofisi ya Hazina, jijini Dar es Salaam ambapo wameangazia mambo mbalimbali ya ushirikiano wa maendeleo.
Dkt. Nchemba ametaja maeneo muhimu ya uwekezaji katika Sekta ya nishati ikiwa ni pamoja na usambazaji wa umeme, kuwekeza katika Mafuta na Gesi kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye akiba kubwa ya hydrocarbon yenye gesi na mafuta.
Alisema kuwa Maendeleo ya miundombinu hiyo ni kipaumbele kikubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania na inatarajia kuwa na matokeo makubwa na ya haraka katika kuongeza ajira na kukuza kipato.
Alisema maeneo mengine muhimu ambayo Serikali imeweka jitihada ni pamoja na Ushirikiano wa Umma na Binafsi (PPPs) katika sekta za uzalishaji ambazo zina jukumu muhimu katika kuendesha maendeleo endelevu nchini.
Aidha Dkt. Nchemba ameziagiza timu za wataalam kuhakikisha zinafanya majadiliano ya kina kuhusiana na uwekezaji ambao taasisi hiyo imeonesha nia ya kufanya uwekezaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya British International Investment, Bw. Simon Cheung, alisema Taasisi yake ipo tayari kufanya majadiliano na Serikali ya Tanzania na kuipa kipaumbele kwenye kusaidia kuwekeza katika maeneo mbalimbali.