![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2023/07/img_1689654177570-1024x474.jpg)
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva ameziomba taasisi mbalimbali pamoja na mashirika binafsi kushirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo wilayani humo na hasa katika sekta ya afya na elimu.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo katika hafla fupi ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali kwaajili ya shule na Zahanati ya Kilondo kutoka kwa taasisi ya kifedha ya CRDB vyenye jumla ya thamani ya sh. Mil. 10.
Imani Mwaisango ni meneja wa benki hiyo tawi la Ludewa ambaye ndiye aliyekabidhi vifaa hiyo kwa mkuu huyo wa wilaya pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius ambapo walikabidhi bati 152 kwaajili ya shule ya msingi Kilondo pamoja na darubini, kitanda cha kujifungulia akina mama wajawazito pamoja na vifaa tiba vinginevyo kwaajili ya Zahanati ya kata ya Kilondo.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo Mwaisango amesema wametoa msaada huo ikiwa ni ishara ya ushirikiano mwema baina ya Benki hiyo, Serikali pamoja na Jamii kwa ujumla kwakuwa kwa kufanya hivyo ni kama sehemu yao ya kugusa jamii na kuleta chachu ya maendeleo katika kazi zao.
Aidha mkuu huyo wa wilaya Victoria Mwanziva ameishukuru benki hiyo kwa mchango huo wenye thamani na wenye kuipa nguvu Serikali kwenye utoaji wa huduma hasa katika upande wa huduma za afya na kwenye kuboresha miundombinu ya Elimu.