Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewaagiza wataalam wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF ),kuhakikisha wanafanya uhakiki kwa kufuatilia wanufaika waliotolewa kimakosa kwenye mpango huo ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza.
Aidha ameelekeza , endapo wapo wanufaika wanaopaswa kutolewa kwenye mradi watolewe kupitia mkutano mkuu wa vijiji badala ya wataalam wachache kujifungua ndani na kuamua kwa matakwa yao kuengeua ama kuingiza wanaowataka wao.
Ridhiwani alitoa maagizo hayo katika ziara yake ,Dunda Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani wakati akizungumza na wataalam na wanufaika wa TASAF.
“Wenye sifa ya kuingia kwenye mradi waingizwe na wanaotakiwa kutolewa watolewe kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa bila kuonea mtu”
“Msiwaondoe watu kwa muonekano wa umaridadi wao,au kigezo cha nyumba ya kuishi hiyo sio alama ya utajiri , unaweza kumtoa mtu wakati bado anauhitaji wa kuendelea kunufaika na mradi'”alisisitiza Ridhiwani.
Vilevile Ridhiwani alieleza kwamba, mradi huo ulianza kipindi kirefu ni kweli wapo waliopiga hatua kiuchumi na kimaisha,wanaweza kusimama wenyewe hivyo wanatakiwa kuondolewa ama kujiondoa ili kupisha wengine wenye uhitaji.
Alibainisha, Serikali ya awamu ya sita imeuendeleza mradi huu wa TASAF kwa kuzingatia hali za kaya hizi, ambapo Rais dkt.Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili ametenga sh. Biln 51 kwa ajili ya mradi huo.
Awali mnufaika WA mradi Bagamoyo, Mwanahawa Hassan alieleza, tayari amejikita kwenye shughuli za ujasirimali na kuwa na mabadiliko kwenye maisha yake hivyo kwasasa anaomba atolewe.
“Nimeshanufaika na mradi, naweza kusimama mwenyewe pia naishukuru Halmashauri kwa kuniwezesha mkopo wa milioni saba ambao umeniinua kwenye biashara zangu .”alieleza Mwanahawa.
Roselyn Kimaro ni mratibu wa TASAF Mkoa wa Pwani anasema, wanafuata maelekezo ya Serikali na wanaendelea kutatua changamoto zilizopo kulingana na maelekezo yanayotolewa na atahakikisha wanasimamia maagizo yanayotolewa.
Alieleza, katika wilaya za Kibaha, Kisarawe na Bagamoyo ni kati ya maeneo yenye wanufaika wa kaya masikini ,wilaya ambazo baada ya kuingizwa kwenye mpango wa TASAF wamekuwa na mabadiliko ya makazi na maisha kwa ujumla.
Awamu ya tatu ya mradi wa TASAF ambayo ilizinduliwa 2020 kiasi cha sh.trilioni 2 zilielezwa kwamba zitatumika kutoa ruzuku kwa kaya masikini pamoja na kuimarisha maisha ya kaya zenye uhitaji kupitia miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na miundombinu .
Kwa mujibu taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2020, Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na umasikini, kina cha umasikini katika Taifa hili la Afrika Mashariki ni asilimia 26.4.
Huku matokeo ya utafiti katika kitabu cha hali ya kiuchumi yanaonyesha umaskini wa mahitaji ya msingi ni mkubwa kwa maeneo ya vijijini kwa asilimia 31.3 ikilinganishwa na maeneo ya mijini ambayo ni asilimia15.8.