Baadhi ya wafugaji wanaofanya shughuli za kifugaji katika kijiji cha Mkwela wilayani Tunduru,wakimsikiliza Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole(hayupo pichani) wakati wa kampeni ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa jamii ya wafugaji.
Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole,akitoa elimu ya kifua kikuu kwa watu wa jamii ya wafugaji katika kijiji cha Mkowela wilayani humo.
Kiongozi wa jamii ya wafugaji wanaofanya shughuli zao katika kijiji cha Mkowela wilayani Tunduru Samwel Mandalu akiomba ufafanuzi juu ya uhusiano kati ya maziwa ya ng’ombe na ugonjwa wa kifua kikuu kutoka kwa Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole wa kwanza kushoto, wakati wa kampeni ya uelimishaji,uchunguzi na uibuaji wa ugonjwa huo.
Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole kushoto,akimsikiliza kiongozi wa jamii ya wafugaji kutoka kijiji cha Mkowela wilayani humo wakati wa kampeni ya uelimishaji,uchunguzi na uibuaji wa kifua kikuu kwa wafugaji.
Kiongozi wa jamii ya wafugaji kutoka kabila ya Wasukuma wanaofanya shughuli za ufugaji kijiji cha Mkowela Samwel Madalu kulia,akimshukuru Mratibu wa ugonjwa wa kifua na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole baada ya kukamilika kwa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WANANCHI wa jamii ya kifugaji wilayani Tunduru,wameiomba serikali kuwasogezea huduma za afya ikiwemo za uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu katika maeneo yao ili kuepusha uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa huo.
Wametoa ombi hilo jana,kwa wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma kutoka Hospitali ya wilaya Tunduru wakati wa kampeni ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa jamii ya wafugaji wanaoishi katika kijiji cha Mkowela wilayani humo.
Samwel Mandalu(65) alisema,wakati umefika kwa serikali kutoa upendeleo kwa kuwajengea zahanati katika maeneo yao ili waweze kupata huduma za afya ikiwemo uchunguzi wa ugonjwa kifua kikuu.
Alisema,kutokana na mazingira na shughuli zao kufanyika mbali na makazi ya watu wengine inakuwa vigumu kufikiwa na elimu ya afya mara kwa mara.
Alisema,watashukuru iwapo serikali itapeleka huduma za afya kwenye maeneo yao ili iwe rahisi kupata elimu juu ya ugonjwa wa kifua kikuu na magonjwa mengine.
Alisema kuwa,wafugaji wengi wanaishi kwenye vitalu maeneo ya porini ambako wanategemea dawa za asili tu kama tiba ya maradhi yao huku baadhi yao hawajawahi kukutana na wataalam wala kufika Hospitali katika maisha yao yote.
Samwel alisema,wafugaji wengi hawajasoma kutokana na muda mwingi wa maisha yao kuishi na mifugo porini,hivyo ni vigumu kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya afya.
Aliongeza kuwa,kama serikali itawafuata kwa kuwapelekea huduma kule waliko itakuwa rahisi wao kuwa na uelewa na kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo.
Studio Samwel,ameishukuru Hospitali ya wilaya Tunduru kupeleka wataalam katika maeneo yao kwa ajili ya kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa kifua kikuu kwani itawawezesha kufahamu madhara na namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Alisema,wafugaji hawafahamu kama maziwa ya ng’ombe yasiyochemshwa vizuri yanaweza kuambukiza kifua kikuu kwa kuwa katika maisha yao wamezoea kunywa maziwa mabichi na kuishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa miti na kuzungushiwa na udongo.
Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,jamii ya wafugaji ni miongoni mwa kundi lililopo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo kutokana na aina ya maisha yao.
Alitaja sababu ya maambukizi kwa wafugaji ni kunywa maziwa yasiyo chemshwa mara kwa mara na kuishi kwenye makazi duni ambayo ni rafiki kwa vimelea vya ugonjwa huo.
Kihongole alitaja makundi mengine yaliyoko kwenye hatari hiyo ni wasafiri,wazee kutokana na kupungua kwa kinga za mwili,wanywaji wa pombe kupindukia, watu wenye magonjwa sugu na ya muda mrefuna watoto wadogo wenye tatizo la utapiamlo.
Amewashauri akina mama wajawazito kujifungulia Hospitali kama njia ya kuwakinga watoto wao baada ya kuzaliwa,watu kula chakula bora chenye mchanganyiko wa aina mbalimbali za vyakula na kuishi kwenye nyumba bora zinazopitisha hewa na mwanga wa kutosha.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa zahanati ya Mkowela Dkt Neema Msangilwa alisema,kwa mwaka 2022 walifanikiwa kuibua wagonjwa 100 wa kifua kikuu.
Alisema,wagonjwa hao walipatikana kupitia kampeni mbalimbali zinazofanyika na wengine walipatikana kupitia dalili zinazoonyesha wanapofika zahanati kwa ajili ya kupata matibabu.
Alisema kijiji cha Mkowela kina zaidi ya watu elfu mbili,hivyo watu 100 wenye kifua kikuu ni wengi mno,ambapo ameiomba serikali kuendelea kufanya kampeni hizo mara kwa mara ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.