Na Victor Masangu, Kibaha
Katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu wadau wa maendeleo na wananchi wa Halmashauri ya Kibaha mji wameungana kwa pamoja kwa lengo la kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa sekondari.
Wananchi hao wakiwemo wadau wa maendeleo,viongozi wa chama Cha mapinduzi (CCM) pamoja na viongozi wa halmashauri ya mji Kibaha wameamua kushikamana bega kwa bega bila kujali itikadi zozote ili kukamilisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari ambayo inatarajiwa kujengwa katika eneo la Mbwate kata ya Mkuza.
Moja Kati ya wadau wakubwa wa maendeleo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ameungana na umati wa wananchi katika halfa maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya uzinduzi wa eneo ambalo litatumika kwa ajili ya ujenzi huo wa shule ya sekondari.
Koka katika halfa hiyo alichangia kiasi cha shilingi milioni moja ikiwa ni ahadi yake ambayo aliweza kuitoa wakati wa zoezi la mchakato wa kuanza kutafuta eneo maalumu kwa ajili ya kuanzisha miradi huo wa shule.
Mbunge huyo alibainisha kwamba pamoja na Rais Samia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo lakini wadau na wananchi nao wameweza kumuunga mkono kwa hali na mali kwa kutoa michango yao mbali mbali ambayo imeweza kusaidia katika kufanikisha jambo hilo.
“Kwanza ndugu zangu nipende kumshukuru sana Rais wetu Mama Samia kwa kuweza kutoa fedha zaidi ya milioni 520 kwa lengo la kujenga shule mpya ya sekondari na mtakumbuka wakati tunaanza mchakato niliahidi milioni moja na leo ninaikabidhi rasmi kwa viongozi wa serikali ya mtaa,”alisema Koka.
Pia Koka aliongeza kuwa pindi mradi huo utakapokuja kukamilika utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa Wanafunzi kuondokana na changamoto ya kutembea umbari mrefu kwani hapo awali walikuwa wanateseka.
Kwa Upande wake Diwani wa kata ya Mkuza Focus Bundala alisema kuwa upatikanaji wa eneo hilo ni ushirikiano mkubwa ambao umefanywa na viongozi mbali mbali pamoja na wananchi lengo ikiwa ni kuanzisha mradi wa ujenzi huo wa shule ya sekondari.
Aidha diwani alifafanua kwamba kwa sasa wanafunzi wa sekondari wanateseka kutokana na kutembea umbari mrefu wa kwenda kupata huduma ya elimu katika shule ya nyumbu hivyo kukamilika kwa ujenzi huo kutakuwa ni mkombozi mkubwa.
Naye afisa elimu sekondari katika halmashauri ya mji Kibaha Rosemerry Msasi alisema kwamba serikali tayari imeshatoa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 520 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mindombinu mbali mbali ya ujenzi wa shule.
Alisema katika mradi huo utakuwa na mindombinu mbali mbali ya majengo ya kisasa pamoja na majengo ya kiutawala hivyo amewataka wananchi wa eneo hilo kuhakikisha wanakuwa ni walinzi wazuri katika kuitunza na kuilinda miundombinu ya majengo ili iweze kudumu kwa miaka mingi.
Mwenyekiti wa chama Cha mapinduzi (CCM) Mwajuma Nyamka alimpongeza mwananchi ambaye alithubutu kutoa eneo hilo lenye ukumbwa wa zaidi ya hekari nne kwa kuona umuhimu katika suala zima la kuwasaidia watoto katika sekta ya elimu.