![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2023/07/IMG-20230713-WA0305-1024x682.jpg)
Na Victor Masangu,Kiluvya
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hashimu Komba ametoa siku 14 kwa mtendaji wa kata ya kibamba kuhakikisha anaanzisha ulinzi shirikishi katika mitaa yote kwa lengo la kukomesha vitendo mbali mbali ya uharifu.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kikazi katika kata ya kibamba kwa ajili ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuweza kusikiliza kero na changamoto ambazo zinawakabili wananchi.
Alisema katika ziara yake katika kata ya kibamba ameweza kubaini kuwepo kwa vijana wengi ambao ni wavuta bangi na baadhi yao hawana kazi za kufanya na kuendelea kujihusisha na vitendo vya uharifu na kuiba vitu mbali mbali katika nyumba za watu.
“Ninatoa siku 14 kwa mtendaji wa kata kuanzisha ulinzi shirikishi katika mitaa yote na hii lengo lake kubwa ni kuweza kupambana na uharifu pamoja na kudhibiti vijana ambao wanajihusisha na madawa ya kulevya kwa hiyo ili Jambo linatakiwa kufanyiwa haraka,”alisema Mkuu wa Wilaya.
Pia aliwataka watendaji kuachana na tabia ya kukaa maofisini na badala yake wanatakiwa kuwatumikia wananchi kwa kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ikiwemo kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo.
Kadhalika mkuu huyo aliwataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwahudumia wananchi pasipo kuomba rushwa ya aina yoyote na kwamba atowafumbia macho wote wenye tabia Kama hiyo.
Katika hatua nyingine amempongeza kwa dhati diwani wa kata ya Kibamba Peter Kilango kwa kuweza kushirikiana na wananchi katika kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo katika nyanja tofauti.
“Kwa kweli nimetembelea miradi mbali mbali katika kata ya kibamba lakini nipende kumshukuru diwani wa kata hii ya kibamba kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo na ninawaomba miradi mingine iendelee kutekelezwa ili wananchi waweze kupata huduma,”alisema.
Nao baadhi ya wananchi ambao wamehudhulia katika mkutano wa adhara wameeleza changamoto zao ikiwemo suala migogoro ya ardhi,miundombinu ya bararabara,pamoja na ukosefu wa kituo cha polisi hasa eneo la hondogo.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo yupo katika ziara ya kikazi kwa ajili ya kuweza kugagua miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa sambamba na kusikiliza kero na changamoto za wananchi.