Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiwasili katika Kijiji cha Potea wilayani Kondoa kwa ajili ya kukagua na kukabidhiwa madarasa yaliyokamilika kupitia mradi wa boost. Wengine katika picha (kulia) ni Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Potea Bw. Iddi Issa Mugubali na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kondoa Bw. Shaban Millao.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiteta na Mwenyekiti wa Kijiji cha Potea wilayani Kondoa kwa ajili ya kukagua na kukabidhiwa madarasa yaliyokamilika kupitia mradi wa boost na kuzungumza na wananchi wa Kijiji hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Amani Abeid Karume (hawapo pichani) iliyopo Pahi Wilayani Kondoa, akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja madarasa yaliyokamilika kupitia mradi wa boost.
Sehemu ya wananchi wa Kijiji cha Potea Wilayani Kondoa wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule aliyefika kijijini hapo kwa lengo la kuzungumza na kutatua changamoto zinazowakabili.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wajumbe wa Baraza la Madiwani (hawapo pichani) katika Wilaya ya Kondoa kupitia na hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Sehemu ya madiwani wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule katika kikao maalumu cha baraza kilichojadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kwa Wilaya ya Kondoa.
Na.Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika kuimarisha miundombinu ya wanafunzi kusoma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za Msingi na Sekondari hivyo wazazi wana wajibu wa kuhakikisha wanafunzi wanakwenda shule na kudhibiti utoro.
Senyamule ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Potea Wilayani Kondoa wakati wa ziara kukagua miundombinu ya madarasa ambayo yamekamilika kupitia mradi wa boost.
“Sote ni mashahidi wa mabadiliko haya katika sekta ya elimu, madarasa mazuri yamekamilika na nyinyi mmechangia hapa nguvu kazi yenu, wazazi tutimize wajibu wetu wa kuwapeleka watoto shule, maana ya madarasa haya ni kuchochea maendeleo na ufaulu” Senyamule amesema.
Aidha, akizungumza pia na jamii ya Kijiji cha Potea Senyamule amewataka kutunza miundombinu hiyo inayogharimu Serikali fedha nyingi na kuwatumia mkutano huo wa hadhara kuwahimiza jamii kutowaficha majumbani watoto wenye changamoto ya ulemavu.
“Mtoto yoyote yule ana haki ya kupatiwa elimu, watoto walemavu pia wana haki sawa na wengine, kuwaweka nyumbani ni kuwa nyanyapaa na kuwanyima haki za msingi
msifiche watoto majumbani, watoeni wapate haki yao ya msingi ya kupata elimu bure inayotolewa na Serikali na madarasa haya yaliyokamilika yana miundombinu rafiki kwa wenzetu wenye changamoto za ulemavu”
Senyamule ametoa rai pia kwa wananchi wa Potea kujikita katika kilimo na kutunza chakula kitakachotosheleza mahitaji ya familia kabla ya kuuza na kusisitiza agenda endelevu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Pia ametembelea Shule ya Sekondari ya Amani Abeid Karume na kuhimiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwapa motisha ya kuandaa ziara ya mafunzo kutembelea miradi ya kimkakati iliyopo katika Mkoa wa Dodoma ikiwa ni pamoja na Mji wa Serikali, Ujenzi wa Mahakama, Barabara za Mzunguko na Reli ya kisasa ya mwendo kasi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ali Gugu amezitaka Kamati za ujenzi kuweka kumbukumbu sahihi za miradi wanayoisimamia baada ya kukamilika kwa ajili ya ukaguzi, kwakuwa ni fursa ya kuongezewa fedha katika sekta nyingine.
Katika Mkutano wa hadhara wananchi wa Potea waiomba Serikali kujenga shule nyingine ya Sekondari katika eneo hilo pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara. Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo Mhe. Senyamule amemwelekeza Afisa Elimu Mkoa na Meneja wa TARURA kufika mapema eneo hilo kufanya tathmini ya hali halisi.