Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Wakili Julius Mtatiro akitoa taarifa ya kukamatwa Ng’ombe zaidi ya 800 katika doria na operesheni mbalimbali za kuondoa mifugo na wafugaji waliovamia kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kufanyika kwa shughuli za ufugaji na yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kijamii wilayani humo.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema,wamekamata zaidi ya ng’omba 800 waliovamia mashamba na kuharibu mazao ya wakulima katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Amesema,ng’ombe hao wamekamatwa kutokana na doria na operesheni kubwa inayoendelea ya kuwaondoa wafugaji wote wanaofanya shughuli za ufugaji na kuingiza mifugo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.
Mtatiro amesema hayo jana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake,na kusisitiza kuwa ni lazima wafugaji wote kwenda katika maeneo(vitalu)vilivyotengwa kwa ajili kufugia mifugo badala ya kuendelea na ufugaji holela.
“kuna tabia ya baadhi ya wafugaji kupeleka kwa makusudi mifugo yao kwenye mashamba na kuharibu mazao ya wakulima jambo linalosababisha migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji hao”alisema.
Kwa mujibu wa Mtatiro,serikali itaendelea kufanya doria na operesheni ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vikosi vinavyofanya kazi ya kuondoa mifugo katika vijiji vyao.
Alisema,mwaka 2019 serikali wilayani Tunduru ilitenga jumla ya vitalu 250 ili vitumike kwa ajili ya ufugaji,hata hivyo ni vitalu 125 tu vimelipiwa na kutumika kwa ajili ya kazi hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya alisema,wamemkamata Afisa mtendaji wa kijiji cha Machemba na Misechela na wenyeviti wa vijiji hivyo,kwa kuruhusu wafugaji kuingiza mifugo kwenye maeneo ambayo hayakutengwa kwa ajili ya ufugaji.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Namasakata wilayani humo wamesema,kata hiyo hakuna vitalu vya mifugo vilivyotengwa kwa ajili ya ufugaji, lakini kuna makundi makubwa ya mifugo.
Diwani wa kata hiyo Rashid Usanje alisema,makundi ya mifugo yanavamia mashamba na kuharibu mazao mashambani na kuiomba Serikali kuchukua hatua kuwadhibiti wafugaji na mifugo yao.