Na Mwandishi wetu, Arusha
BAADHI ya jamii nyingi za vijijini nchini Tanzania zina changamoto mbalimbali za kunyang’anywa ardhi zinazofanana kutokana na makampuni ya wawekezaji na uchimbaji madini.
Ofisa wa shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini Joyce Ndakaru amesema amejionea namna wanaume na wanawake ambao ni wasaidizi wa jinsia na ardhi wanavyoweza kusaidia.
Kwa muda wa miezi minane iliyopita amekuwa akizunguka katika jamii za kaskazini mwa Tanzania na wasaidizi wa jinsia na ardhi walionufaika kupitia mradi wa kimataifa wa Usalama wa Umiliki wa Ardhi kwa Wanawake (Women’s Land Tenure Security-WOLTS), ambao shirika la HakiMadini, linashirikiana na Mokoro ya Uingereza na People Centered Conservation-PCC ya Mongolia.
Ndakarau na wenzake walishirikisha kile walichojifunza kupitia mpango wa mafunzo ya jinsia na ardhi kwa jamii nyingine, kuhusu sheria ya ardhi na haki za wanawake na waliweza kuelimisha na kuhamasisha jamii zote walizozitembelea.
Amesema katika kila kijiji changamoto zilifanana; wawekezaji walikuwa wakija na karatasi za serikali na vibali vinavyowapa haki ya kutafuta rubi au madini mengine, na wanakijiji hawakujua ni haki gani walikuwa nazo kulinda ardhi na maisha ya jamii zao.
Anasema mmoja wa wasaidizi wa jinsia na ardhi, Salome Peter, alikuwa akiwasihi wanawake wasiogope.
Amekutana na mwanaume wa kimasai mwenye moyo mkunjufu na uzoefu wa miaka mingi kama kiongozi wa mila na mwenyekiti wa zamani wa kijiji, alikuwa amepata ujasiri zaidi baada ya kuchaguliwa na jamii yake kushiriki katika programu ya mafunzo kuhusu jinsia na masuala ya ardhi.
Ana uwezo wa kuzungumza kwa urahisi kuhusu haki za jamii wakati wachimbaji wanapofika kwenye ardhi yao na kueleza taratibu sahihi za kufuata ili kuhakikisha kila mtu ananufaika na kwamba watu wanyonge hawadhulumiwi.
Pia ana madokezo mazuri juu ya nini cha kufanya ikiwa wachimbaji wa madini wataanza ghafla kulima ardhi jambo ambalo limetokea katika maeneo zaidi ya moja waliyoyatembelea.
Msaidizi mwingine wa jinsia na ardhi, Sindooi Mollel, amewavutia wanawake na wanaume kwa mtazamo wake wa kujiamini kuhusu haki za ardhi za wanawake.
Akiwa mjane katika umri mdogo, Sindooi alikuwa ametumia ujuzi wake mpya aliopata kupitia programu ya mafunzo ya jinsia na ardhi ya WOLTS kupata urithi wake.
Pia amechaguliwa na jamii yake kushiriki mafunzo na amekuwa mstari wa mbele na sauti katika kutetea haki za ardhi za wanawake na kupinga unyanyasaji wa kijinsia (GBV) wa kila aina.
Peter amemuunga mkono Sindooi, akizungumzia dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kushawishi utoaji wa haki kwa wajane na wanawake ambao hawana watoto.
Ametolea mfano mti mkubwa uliowafunika washiriki wote kutokana na jua kali katika kijiji kimoja, aliona kwamba miti isiyo na matunda ingali na manufaa mengi kwa watu wa jamii hiyo.
“Mimi mwenyewe kama mwanamke wa Kimasai, niliweza kuona kwamba Peter na Sindooi na wasaidizi wetu wengine wa jinsia na ardhi, Milya na Rosa, hawakuwa wakieleza tu mambo ya kitaalamu kama vile sheria ya ardhi na dhana za jinsia, bali waliweza kuyatafsiri katika lugha yao,” amesema.
Amesema kila siku ambayo watu wangeweza kuelewa na hawakuogopa kuzungumza juu ya masuala ambayo wasingeweza kamwe kuthubutu kuyaibua.
Amesema Sindooi alizungumza waziwazi kuhusu wanaume kuzitelekeza familia zao, na kuwa na mahusiano nje ya ndoa zao na wanawake walilazimika kuishi kama wajane ingawa waume wao walikuwa bado wangali hai.
Amesema alipokuwa akiongea, wanaume wengi walikuwa wakitazama chini, wakichukua ujumbe wake wenye uchungu na walipoondoka wakahisi kwamba kumekuwa na uhusiano wa kweli na jamii.
“Nimekuwa nikifanya kazi ya haki za ardhi na uchimbaji madini nchini Tanzania kwa miaka mingi, lakini mradi huu umenifungua macho kuona uwezekano wa wasaidizi wa jinsia na ardhi wa ndani ya jamii kufanya mabadiliko ya kweli,” amesema.
Amesema kwa kuzipa jamii nafasi ya kujifunza kuhusu haki zao na kisha kuchagua watetezi wao wenyewe, wanaonekana kuwezeshwa zaidi kuliko watu wa nje wanapokuja kwa safari fupi kutoa mafunzo au ushauri.
“Kilichoanza kama mradi kuhusu haki za ardhi za wanawake pia kimekuwa zaidi na masuala nyeti ambayo hayangezungumzwa nilipokuwa msichana, leo yanazungumzwa mbele ya wanaume na wanawake wa rika zote,” amesema.
Amesema wasaidizi wapya wa jinsia na ardhi wanatambuliwa na njaa ya maarifa katika jamii itawasukuma mbele zaidi.
Amesema kuondoka kwenye vijiji walivyotembelea pamoja na wasaidizi wa jinsia na ardhi, ana imani kuwa mabadiliko ambayo jamii inayataka yataendelea kwa muda mrefu.