David Luya mkazi wa mtaa wa Naazaret Halmashauri ya wilaya Tunduru kushoto akiomba msamaha baada ya kukamatwa na mkuu wa wilaya ya Tunduru wakili Julius Mtatiro baada ya kukutwa na mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 12 (jina na shule linahifadhiwa) chumbani kwake majira ya saa 5.30 usiku kinyume cha sheria.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro kulia,akimuhoji David Luya mkazi wa mtaa wa Nazareti wilayani humo baada ya kukutwa ana mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 12 chumbani kwake majira ya saa 5.30 usiku bila ridhaa ya wazazi wake.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro kwa kushirikiana na jeshi la polisi,wamefanikiwa kumkamata David Luya mkazi wa mtaa wa Nazareti wilayani humo akiwa na msichana mdogo mwenye umri wa miaka 12(jina linahifadhiwa)ndani ya chumba chake.
Akizungumza jana na waandishi wa Habari katika eneo la tukio Mtatiro alisema,Luya amekamatwa majira ya saa 5.30 usiku akituhumiwa kujihusisha kimapenzi kwa muda mrefu na msichana huyo anayesoma shule ya moja ya sekondari jijini Dar es slaam.
Alisema,vyombo vya ulinzi na usalama vilipata taarifa kwamba katika mtaa wa Nazaret kuna mwanaume mtu mzima amekuwa akijihusisha kimapenzi na kuwadhalilisha wasichana wadogo mara kwa mara.
Mtatiro alisema,waliweka mtego na walipofika katika nyumba hiyo walimkuta mtuhumiwa akiwa na mwanafunzi chumbani kwake bila ridhaa ya wazazi.
Alisema,baada ya kuwakamata wote wawili kwenye simu ya mtuhumiwa ilikutwa picha ya video ikimuonyesha msichana huyo mdogo akiwa chumbani kwa mtuhumiwa akitumikishwa kingono.
Alieleza kuwa,baada ya kufikishwa kituo cha Polisi msichana huyo alikiri kuwa amekuwa akitumikishwa kingono na mtuhumiwa kwa muda mrefu pindi wazazi wake wanapoondoka.
” na hata baada ya binti kufanyiwa vipimo vya kitaalam ilibainika kwamba ameingiliwa kingono na sasa taratibu za kumfikisha mahakamani mtuhumiwa zinaendelea”alisema.
“huyu mtuhumiwa siyo mwenyeji wa hapa, nadhani mwenyeji wa mkoa wa Singida ambaye amekuja Tunduru kujihusisha na masuala ya utafiti wa kilimo,lakini tulipewa taarifa kwamba amekuwa na mienendo siyo mizuri kwa muda mrefu na jana ndiyo tumefanikiwa kumkamata”alisema.
Katika hatua nyingine Mtatiro alisema,kukamatwa kwa Luya kumetokana na operesheni kali inayoendelea wilayani humo ya kuwasaka wanaume wanaojihusisha na kimapenzi na wasichana wenye umri mdogo hasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kusababisha watoto wengi wa kike kuacha shule.
Pia alisema,msako huo unawahusu wazazi wote wanao wakatisha watoto masomo na kuwatumikisha kazi mbalimbali na wanaoozesha watoto wa kike katika umri mdogo kwa tamaa ya kupata fedha za mahali.
Kwa upande wake David Luya,alikataa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi huyo na alikwenda chumbani kwake kuazima simu ili kumpigia dada yake aliyekuwa kwenye shughuli zake za biashara.
Dada wa msichana huyo Sabrina Abdala alisema,alipata wasiwasi na mdogo wake kuwa na mahusiano baada ya kumuona akiwa na simu ya mtuhumiwa.