Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka akimsaidia Bi Sophia Ali baada ya kumpatia Baiskeli ya magurudumu matatu ili imsaidie katika shughuli zake za kila siku.
Mkazi wa mtaa wa Muungano Tunduru Sophia Ali kulia mwenye ulemavu wa miguu,akifurahia jambo na Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka aliyekwenda nyumbani kwa Sophia kukabidhi msaada wa fedha taslimu Sh.500,000.
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka kushoto,akisalimiana na mkazi wa mtaa wa Muungano Halmashauri ya wilaya Tunduru Sophia Ali na mtoto wake Rukia Hausi ambao wote ni walemavu wa miguu kabla ya kutoa msaada wa Sh.500,000 ili ziweze kuanzisha biashara ndogo ndogo.
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka wa pili kulia,akikabidhi kiasi cha Sh.500,000 kwa familia ya Bi Sophia Ali kushoto wenye ulemavu wa miguu ili ziweze kuwasaidia kuanzisha biashara ndogo ndogo.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka,ameifuta machozi familia ya Sophia Ali mkazi wa mtaa wa Muungano Halmashauri ya wilaya Tunduru yenye walemavu watatu baada ya kuwakabidhi jumla ya Sh. laki 5 ili ziwasaidie kupata mahitaji yao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Nyoka alisema,fedha hizo ni kwa ajili ya mtaji wa kuanzisha biashara ndogo ndogo ambayo itawawezesha kupata mahitaji yao ya kila siku kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Alisema,hiyo siyo mara ya kwanza kutoa msaada kwa familia hiyo ambapo awali alitoa baiskeli ya magurudumu matatu kwa Sophia ili iweze kumsaidie katika shughuli zake za kawaida.
Alisema,kama Mbunge ana wajibu wa kuwasaidia watu mbalimbali waliopo katika jamii na ni fahari kubwa kwake kuona ametimiza ahadi yake kwa familia hiyo.
“nitaendelea kuisaidia jamii ya watu wenye mahitaji muhimu kadri nitakavyoweza,hii siyo mara yangu ya kwanza kutoa msaada kwa familia ya Sophia Ali,mwezi Machi nilikabidhi baiskeli ili iweze kumsaidia mama yetu katika shughuli zake za kila siku”alisema.
Aidha,amewaomba viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuwa na utaratibu wa kuwaibua na kuwatambua watu wenye mahitaji maalum waliopo katika jamii ili waweze kusaidiwa.
Alisema,hatua hiyo itasaidia sana watu hao bila kujali itikadi za vyama kupata msaada kutokana na mahitaji yao na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili kuisaidia familia hiyo yenye changamoto nyingi za maisha.
Akizungumza huku akitokwa na machozi ya furaha Sophia Ali amemshukuru Mbunge huyo kuwapatia msaada huo na kueleza kuwa,atatumia fedha hizo kwa ajili ya kuanza kujenga nyumba kuishi.
Alisema,kwa sasa anakabiliwa na hali ngumu ya maisha yeye na familia yake kwani sehemu kubwa ya maisha yao wanategemea kupata ridhiki kupita mitaani kwa ajili ya kuomba,na kuwaomba watu wenye uwezo kuwasaidia.
Kwa upande wake katibu wa Jumuiya ya umoja wa wanawake(UWT)wilayani Tunduru Clementina Kasajo, amehaidi kuwa karibu na familia hiyo ili fedha na misaada inayotolewa na wadau kwa ajili ya familia hiyo zifanye kazi inayokusudiwa.
Mwenyekiti wa UWT wilayani humo alisema,hiyo ni mara ya kwanza tangu aingie madarakani kuona Mbunge wa viti maalum kuwajali na kuwatambua watu wenye mahitaji maalum na kuwapatia msaada.