Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa JKT Mhe. Innocent Bashungwa ,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelekea Kilele cha maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT yatakayofanyika Julai 10, 2023 jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kilele cha maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT yatakayofanyika Julai 10, 2023 jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa leo Julai 8, 2023 jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa JKT Mhe. Innocent Bashungwa wakati akizungumza na waandishi wa habari .
Ameongeza kuwa “ Maandalizi yote muhimu kwa ajili ya maadhimisho hayo yamekamilika napenda pia kuwashukuru JKT kwa maandalizi ya maadhimisho haya, wadhamini na wote walioshirikiana nasi katika maandalizi yote
“Kwa namna ya kipekee niwashukuru Uongozi wa Mkoa wa Dodoma chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule kwa uratibu unaoendelea kwa kufanikisha maadhimisho haya ya kihistoria” amesema Mhe. Bashungwa.
Amesema katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma siku ya jumatatu Julai 10, 2023 shughuli zitaanza mnamo majira ya saa 12 : 30 asubuhi na kuhudhuriwa na viongozi wa kiserikali na taasisi mbalimbali na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.
“Karibuni ndugu wananchi kumsikiliza Rais wetu mpendwa na kujionea gwaride la vijana wa JKT, maonyesho ya vifaa mbalimbali vya SUMAJKT, burudani za ngoma kutoka vikundi vya JKT na wasanii mbalimbali” amesema.
Amesema kilele hicho kilitanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na JKT Marathon 2023 iliyofanyika june 25, 2023 kwenye viwanja vya Jamhuri Dodoma ambayo ilikuwa marathoni ya kwanza kuandaliwa na JKT tangu kuanzishwa kwake.
Shughuli nyingine amezitaja kuwa ni uzinduzi wa maonyesho ya kazi na bidhaa zinazozalishwa na JKT sambamba na uzinduzi wa Mnara wa kumbukumbu ya JKT kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake shughuli zilizozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango Julai mosi, 2023.
“Pia mbali na hilo tumefanya shughuli za kijamii kama kufanya usafi na kutoa zawadi katika wodi ya wazazi Hospitali ya Uhuru Chamwino Dodoma pamoja na kutembelea vituo vya kulelea watoto yatima na wenye mahitaji maalumu” amesema.
Katika hatua nyingine Mhe. Waziri Bashungwa amempongeza Rais Samia kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kuhakikisha JKT inaendelea kuwa kitovu cha malezi bora kwa vijana wa kitanzania.