Na Alex Sonna-DODOMA
Wachezaji wa zamani wa mpira wa miguu katika timu za majeshi wamepongeza Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa kuandaa bonanza maalumu lililowakutanisha wachezaji wa zamani wa timu za majeshi huku pia wakipongeza hatua ya Jeshi kupandisha timu mbili za majeshi kucheza ligi kuu ya Tanzania bara NBC.
Wakizungumza wakati wa bonanza hilo maalumu lililoandaliwa na JKT kama moja ya shughuli kuelekea maadhimisho ya kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka Julai 10, 1963.
Wachezaji hao wamesema ni hatua nzuri kwa Majeshi kuwa na timu za ligi kuu kwani miaka ya nyuma Majeshi yalikuwa na timu nyingi na hii inasaidia kuibua vipaji vingi vya michezo mbalimbali na kupata ajira hali inayosaidia kupunguza tatizo la ajira.
“Tunawashukuru JKT kwa kuandaa bonanza hili limesaidia kutukutanisha wachezaji wa zamani tuliochezea timu za majeshi kuna watu tumepotezana muda mrefu kama miaka 20 hivi tangu tulivyoachana kwenye timu tulizozichezea” amesema Lubigisa Madata, mchezaji wa zamani wa 82 Rangers na Simba Sport Klabu.
Kwa upande wake Naverine Kanza aliyewahi kuichezea Klabu ya Transcamp amesema Jeshi ni sehemu sahihi ya kukuza Vipaji vya wanamichezo kwani wanapokea vijana wenye umri mdogo hivyo wakitumia nafasi hiyo wataibua wanamichezo wazuri wa michezo mbalimbali.
Akifungua Bonanza hilo Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Jeshi la Kujenga Taifa JKT Kanali Issa Mlay amesema lengo la bonanza hilo ni kushirikiana na jamii pamoja na wanamichezo mbalimbali katika kubadilishana mawazo na kuimarisha mahusiano katika michezo.
Amesema Bonanza hilo ni mwendelezo wa shughuli zinazofanywa na JKT kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa JKT ambapo walianza na Marathon iliyofanyika June 25, 2023 ikifuatiwa na uzinduzi wa maonyesho ya kazi za JKT na uzinduzi wa Mnara Maalumu Kumbukumbu ya miaka 60 ya JKT na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Nae Katibu wa kamati ndogo ya Maadhimisho ya miaka 60 ya JKT Kaptein Godwin Ekingo amesema bonanza hilo linashirikisha timu tatu ambazo ni JKT Veterani, Twalipo Vetereni kutoka Dar es saalam na Watumishi Vetereni ambapo mshindi wa kwanza na wa pili watapatiwa zawadi siku ya kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya JKT yatakayofanyika Julai 10, 2023.