Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Shule za Sekondari 92 pamoja na Shule za Msingi 154 Mkoani Pwani,zimeanza kilimo Cha mbogamboga ili kukabiliana na changamoto ya chakula shuleni.
Inaelezwa hatua hiyo inakwenda kuchagiza mwamko wa elimu inayoendana na afya bora mashuleni.
Akielezea namna sekta ya elimu mkoa wa Pwani inavyokabiliana kutatua changamoto mbalimbali kwa wanafunzi ili kuhakikisha inainua kiwango Cha ufaulu na kuongeza ari ya kusoma , Sara alitaja aina ya mbogamboga zinazolimwa kuwa ni mikunde,maboga,mchicha,spinach ,matembele ,bamia na nyanya chungu.
Alielezea kwamba, kilimo hicho kinasaidia suala la lishe mashuleni huku jamii ikijifunza kilimo cha mbogamboga kupitia shule hizo.
Aidha Sara alieleza, lishe bora ni suala muhimu kwa afya ya wanafunzi na ni kichocheo cha kusoma kwa bidii.
“Kipindi cha miaka ya nyuma ukosefu wa chakula shuleni ulisababisha utoro na wanafunzi wengine kushindwa kuendelea na masomo kwa kushindwa kuhimili njaa “
Alizitaka shule Mkoani humo kuendelea kuunga mkono mradi wa shule bora ambao umekuwa ukisisitiza umuhimu wa chakula shuleni ili kuinua ufaulu na taaluma kwa wanafunzi.
Sara alihimiza , ulimaji wa bustani na upandaji wa miti ya matunda upewe kipaumbele na kumjengea mtoto tabia ya kulima mbogamboga , matunda tangu akiwa shuleni.
“Lishe ni suala mtambuka ambalo linachagiza wadau wa elimu, wazazi,walezi na jamii ,kuchangia chakula sanjali na shule kuanzisha bustani za mbogamboga ikiwa ni mbinu ya kuondoa tatizo la wanafunzi kushinda bila kula wakiwa shuleni “alisisitiza Mlaki.
Akikazia juu ya suala hilo, Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, anahamasisha elimu itolewe kuhusu lishe kwa manufaa ya watoto na vizazi vijavyo.
Alihimiza ,jamii kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi ili kupambana na changamoto ya mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kuboresha Mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa Halmashauri kuweka kwenye bajeti fedha za ujenzi wa miundombinu.
Ofisa elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Mkuranga ,Jessy Mpangala nae alieleza, wamefanikiwa kutokomeza utoro wa kudumu na wa rejareja kwa kuwapatia watoto chakula shuleni na kuanzisha mashamba darasa ya mbogamboga na mazao ya muda mfupi na mrefu.
Jessy aliongeza kusema, Jumla ya shule 30 zinatekeleza mkakati huo na kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula shuleni na kuhudhuria masomo bila kukosa .
Miriam Kihiyo ni ofisa elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Chalinze anaeleza, Halmashauri hiyo imeanzisha kilimo Cha mbogamboga katika shule za awali na Msingi 12 ,lengo likiwa kusaidia lishe mashuleni ,ili wanafunzi wasome wakiwa na afya njema.
Kihiyo alieleza, mradi wa shule bora kwa kushirikiana na Serikali unaelekeza umuhimu wa lishe mashuleni ili kujenga afya bora kwa watoto hao.
Mradi wa shule bora ,unatekelezwa kwa msaada wa Serikali ya watu wa Uingereza “UKaid” wakishirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) ,katika mikoa Tisa ya Tanzania Bara ikiwemo Pwani, Tanga,Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi, Simiyu, Mara na Rukwa.