Wakili Alex Mgongolwa (kushoto) na Wakili Francis Stolla (kulia) wakiwa katika majadiliano maalumu yaliyoendeshwa katika Ukumbi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) jijini Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hajavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuongezea muda wa kuendelea kukaa ofisini Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma baada ya kutimiza miaka 65.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 3 Julai, 2023 na Wakili Alex Mgongolwa na Wakili Francis Stola wakati wa majadiliano maalumu yaliyoendeshwa katika Ukumbi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) jijini Dar es Salaam.
“Hakuna maneno kwenye Katiba yanayosema Jaji Mkuu akifikisha umri wa miaka 65 hawezi kuongezewa muda wa kuendelea kukaa ofisini. Kumbakiza Jaji Mkuu kwenye kiti chake, au kumfanya aendelee kukaa kwenye ofisi yake siyo kinyume na Katiba, bali ni kwa mujibu wa Katiba hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Wakili Msomi Stola.
Kauli ya Mawakili hao inakuja siku chache baada ya maneno kusambaa kwenye mtandao wa kijamii kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amevunja Katiba kwa kumwongezea Jaji Mkuu wa Tanzania muda wa kukaa ofisini baada ya kufikisha umri wa miaka 65.
Wamesema kuwa hakuna Ibara, wala maneno yoyote katika Katiba yanayosema umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu, ukienda kusoma kwenye Ibara inayohusu umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani, yanayohusiana na kumbakisha Jaji wa Mahakama ya Rufani hayatatumika kwa Jaji Mkuu.
“Vinginevyo, watunga Katiba wangekusudia hivyo wangesema umri wa kustaafu Jaji Mkuu ni sawa sawa na ule a Jaji wa Mahakama ya Rufani, isipokuwa kuendelea kukaa kwenye ofisi [(Kwa mujibu wa Ibara ya 120(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977] haitamhusu Jaji Mkuu,” Wakili Msomi Stola amesema.
Mawakili hao wamebaisha kuwa Ibara ya 118 (2) haitamki miaka ya umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu wala Jaji wa Mahakama ya Rufani, bali umri wa kustaafu kwa viongozi hao unapatikana kwenye Ibara ya 120 ya Katiba ibara ndogo ya kwanza, yaani 120(1) inayosomeka hivi;120(1) ‘Kila Jaji wa Rufani atalazimika kuacha kazi yake ya Rufani atakapotimiza umri wa miaka sitini na tano, LAKINI masharti ya Ibara hii ndogo yatatumika BILA KUATHIRI masharti yafuatayo katika Ibara hii.’
“Kwa hiyo ili uweze kujua umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani lazima uende kwenye Ibara ya 120 (1) ambayo imetamka miaka 65 kama kiwango cha chini na ndio maana kuna kiunganishi cha neno lakini…, ili kuruhusu mazingira mahsusi,” amedokeza Wakili Msomi Mgongolwa.
Aidha, Mawakili hao wamesema Ibara hiyo ya 120 ya Katiba inapaswa kusomwa sambamba na Ibara zake ndogo.
Wamesema ukisoma Ibara ya 120(3) ambayo inasomeka hivi; 120(3) ‘Iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya Manufaa ya Umma inafaa Jaji wa Rufani aliyetimiza umri wa miaka sitini na tano aendelee kufanya kazi, na Jaji huyo wa Rufani anakubali kwa Maandishi kuendelea kufanya kazi, basi Rais aweza kuagiza kuwa Jaji huyo wa Rufani aendelee kufanya kazi kwa muda wowote atakaoutaja Rais.’
Ibara hii ya 120(3) inabainisha wazi kuwa kama kwa manufaa ya umma, Rais ataona Jaji wa Mahakama ya Rufani anapaswa kuendelea, ataelekeza hivyo na Jaji mhusika atakubali kwa maandishi.
“Hivyo umri wa Jaji Mkuu wa kustaafu utaupata kwenye Ibara ya 120 kwa kusoma ibara zake ndogo na sio kuishia kwenye Ibara ya 118(2) peke yake. Hivyo, kuna uwezekano kwa Jaji Mkuu kuwa ofisini akiwa zaidi ya umri wa miaka 65. Hakuna katazo hilo kwenye Katiba,” Wakili Msomi Stola amesisitiza.
Mawakilili hao pia wametoa mfano wa mwaka 2005 ambapo Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa alimwongezea aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wa kipindi hicho, Mhe. Barnabas Samatta, kubaki kwenye wadhifa huo kuendelea kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji Mkuu kwa kipindi cha miaka miwili. Kinachoshangaza sasa ni kwamba imekuwaje baadhi ya watu wamesahau rejea hii ya mwaka 2005 na inakuwaje watu wachache wanaupotosha Umma kwa kusoma Ibara moja tu ambayo Ibara yenyewe haitaji hata umri wenyewe.