Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali Mhe. Francis Mtega, Katika uwanja wa mpira wa Chimala Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya Julai 04, 2023 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……..
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wana-Mbarali wamuombee na kuenzi mazuri yote aliyofanya enzi za uhai wake aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Mhe. Francis Mtega.
Hayo yamesemwa leo (Jumanne, Julai 4, 2023) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipoongoza waombolezaji kuaga mwili wa Mheshimiwa Mtega katika uwanja wa mpira wa Chimala, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia anamfahamu Mheshimiwa Mtega kutokana na uhodari na uwezo wake wa kusimamia ajenda muhimu za wana-Mbarali na za kitaifa katika kipindi chote cha utumishi wake akiwa Mbunge.
“Pamoja na salamu hizo za pole za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, ninaungana naye kuendelea kuwasisitiza kumuombea Mheshimiwa Mtega na kuenzi yote mazuri aliyofanya ili iwe alama ya kumuenzi na kumuombea wakati wote.”
Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa Bunge limeumizwa na kifo cha Mheshimiwa Mtega kutokana na mchango wake mkubwa kwa Wana-Mbarali.
“Mheshimiwa Mtega alikuwa mtu mpole, mstaarabu na mfuatiliaji wa ajenda zote za Wana-Mbarali, alikuwa ni mtu mwema.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda amesema kuwa alimfahamu Mheshimiwa Mtega kutokana na ushujaa na uhodari wake wa namna alivyokuwa akiwatetea wana-Mbarali likiwemo suala la GN.
“Kutokana na juhudi zake, nilikiri kwamba huyu ndiye mwakilishi wa wananchi. Alikuwa ni shujaa, jambo hilo ni zito, halihimiliki lakini tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atutie nguvu.”
Marehemu Mtega alifariki Julai mosi, 2023 kwa ajali ya kugongwa na trekta shambani kwake Mbarali, mkoani Mbeya.