Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Manyara, Inyasi Amsi amewataka vijana nchini kutokuwa vikaragosi wa wanasiasa wanaowatumia kwa maslahi yao binafsi.
Inyasi akizungumza kwenye kikao cha baraza la UVCCM wilaya ya Simanjiro kilichofanyika mji mdogo wa Mirerani amesema vijana wanapaswa kujitambua na kutotumika hovyo na wanasiasa wenye hila.
Amesema vijana nchini wanatakiwa kutambua kuwa viongozi waliopo madarakani wanapaswa kutetewa na kupewa ushirikiano kwani wanatekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025.
“Endapo kuna mwanasiasa ananyemelea nafasi ya ubunge, udiwani au uenyekiti wa mtaa, kijiji au kitongoji, wasubiri kwani sisi tunatembea na viongozi waliopo madarakani na siyo vinginevyo,” amesema Inyasi.
Amesema baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa madaraka waliopo jikoni wasubiri kwani hivi sasa vijana wapo tayari kuwatetea na kuwasemea viongozi waliopo madarakani.
“Mimi siyo kikaragosi au mfuasi wa mwanasiasa yeyote yule asiye madarakani, nanyi muige hivyo msikubali kurubuniwa kwani anayetaka madaraka, asubiri uchaguzi mkuu mwaka 2025 agombee,” amesema Inyasi.
Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Simanjiro, Timoth Mollel amesema agenda kubwa ya baraza lao ilikuwa kumpitisha katibu hamasa na chipukizi Matei Damas uzinduzi wa shina tawi la Songambele na kupokea taarifa ya kamati ya ujenzi wa jengo la UVCCM la wilaya.
“Pia tumegawa kadi kwa wanachama wapya na vijana kupaza sauti zao kwa mbunge ili awapambanie kupata ajira katika kampuni ya Franone Mining LTD na maeneo mengine,” amesema Mollel.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema vijana wasijione wanyonge, watembee kifua mbele kwani Taifa linawategemea.
Mbunge wa viti maalum (vijana) Asia Halamga amewataka vijana wachangamkie fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo, wenyeviti wa UVCCM wa wilaya nne, Hamza Mngia (Kiteto), Elisante Shauri (Mbulu), Justin Ammi (Hanang’) na Solomon Mpaki (Babati vijiji) walishiriki baraza hilo.