Na Jozaka Bukuku
WAKATI habari zikisema kwamba, mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ameugomea mshahara wa zaidi ya Sh34 Milioni alizoahidiwa kulipwa ilimradi abakie klabu hapo, uongozi umebainisha kwamba, unapambana kumbakiza.
Nyota huyo aliyemaliza msimu uliopita kama kinara wa mabao wa Kombe la Shirikisho Afrika akifunga saba na kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akifunga 17 sawa na Saido Ntibazonkiza wa Simba, imeelezwa anataka kuondoka baada ya kupata ofa zenye donge nono nje ya Tanzania.
Mayele mwenye mkataba wa mwaka mmoja na Yanga amegoma kusaini mkataba mpya ambao ungemfanya awe analipwa fedha ndefu kuliko mchezaji yeyote ndani ya timu hiyo huku akidaiwa amepagawa na ofa nono kutoka Esperance ya Tunisia, Zamalek na Pyramids za Misri.
Mayele na Yanga wamekaa vikao visivyopungua vitatu tangu kumalizika kwa ligi ili kuboresha mkataba wake, lakini hakuna mabadiliko yaliyokamilika hadi sasa kwa vile straika huyo kukomaa kutaka aachiwe aende kwenye klabu nyingine.
Yanga ilimpa Mayele ofa ya kumuongezea mshahara kutoka kiwango anacholipwa sasa cha Dola 9,000 (zaidi ya Sh 20 milioni) hadi kufikia dola 15,000 (zaidi ya Sh 34 Milioni), lakini staa huyo amechomoa, japo inaelezwa mazungumzo baina yao yanaendelea ili kupata muafaka.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinalidokeza kwamba siku tatu zilizopita Mayele alienda kambi ya Yanga, iliyopo Avic Town, Kigamboni na kuchukua kila kitu chake jambo lililoongeza hofu kwa Yanga juu ya kumbakiza.
Hata hivyo, katika moja ya mahojiano ya Rais wa Yanga, Hersi Said akizungumzia kuhusu Mayele alisema;
“Mayele ni mchezaji bora na ninafurahia kuona anahusishwa na timu nyingine, hii inaonyesha kuwa Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wakubwa. Kama atakuwa anataka kuondoka, tutaangalia vitu vitatu, moja tutataka kumbakiza, mbili tutaangalia bei nzuri, tatu ni nani atachukua nafasi yake.”
Hersi alibainisha kwamba, kwa namna yotote wanapambana kumbakiza Mayele kwani ni mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa kikosi hicho.
Straika huyo alijiunga Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2021/2022 kwa Mkataba wa miaka miwili, na baadae kusaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja utakaotamatika 2024, hivyo timu yeyote itakayomtaka italazimika kununua mkataba huo.
Mwisho.