Diwani wa kata ya mwisi (ccm) wilaya ya igunga mkoani tabora Ahmed Ibrahim Jambeck (kulia) akibadilishana mawazo na mwanachama wa chama cha demokrasia na maendeleo chadema kata ya Mwisi George Shilinde Maige (kushoto) katika moja ya jengo la vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari mwisi kata ya mwisi.
Diwani Wa Kata Ya Mwisi (Ccm) Wilaya Ya Igunga Mkoani Tabora Ahmed Ibrahim Jambeck Kushoto Akiwa Pamoja Na Mwanachama Wa Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo Chadema Kata Ya Mwisi ,George Shilinde Maige (Kulia) Wakichanganya Zege Katika Ujenzi Wa Moja Ya Bweni La Shule Ya Sekondari Kata Ya Mwisi
Na Lucas Raphael,Tabora.
WANANCHI wa Kata ya Mwisi Wilayani Igunga Mkoani Tabora, wameipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule ya Sekondari ya Mwisi kiasi cha shilingi milioni 642 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa Nane, mabweni Matatu na Matundu 12 ya vyoo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kijijini hapo wananchi hao waliojitambulisha kwa majina ya Cosmas Kalwisha na George Maige ambao ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Asha Jumi na Kwinde Tungu, wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha Kata hiyo za ujenzi wa madarasa na kwa kuendelea kutatua changamoto katika sekta ya Elimu, Afya na Maji jambo ambalo limewapa matumaini makubwa na kuendelea kuiamini Serikali ya awamu ya Sita.
” Mimi pekee natanguliza shukrani zangu za dhati kwa mama yetu Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kwa jitihada anazozifanya, nikizungumzia kata ya Mwisi kuna fedha zimetolewa kama milioni 642 na sasa hivi kazi inaendelea pale shuleni ya kujenga madarasa, mabweni na matundu ya vyoo yaani kazi inafanyika nzuri sana kiasi kwamba hata ukifika wakandarasi wanafanya kazi muda wote pia diwani Jambeck na walimu wanasimamia kazi muda wote,” alisema Kalwisa (CHADEMA).
Huku George Maige akisema kuwa, ” Mimi ni Mwanachadema, katika miradi ya maendeleo ni lazima tuseme ukweli nikianzia katika Elimu, siku za nyuma tulikuwa tunachangishwa fedha kila kaya lakini majengo yalikuwa hayaendi, lakini katika utawala wa Rais Samia madarasa, mabweni yanaota kama uyoga, leo nimetembelea hapa shuleni nimeona kazi zinapigwa, kwa kweli inatia moyo sana, ili kuwa na maendeleo bora inaitaji kuwa na viongozi bora, huku wakimpongeza pia diwani wa kata yao Ahmed Ibrahim Jambeck kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kuisimamia fedha inayoletwa katika kata yao ya Mwisi.
Aidha, Asha na Kwinde, wamewataka Wananchi wenzao kushirikiana na wanafunzi na walimu kusimamia miradi hiyo na kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu, na kuhakikisha kuwa atakaye ihujumu basi anakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Ahamed Jambeck, alimpongeza Rais Samia kwa kuwaamini watendaji wake katika ngazi ya chini na kuendelea kuwapatia fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya, elimu, maji na umeme.
” Kwanza kabisa nitoe shukrani zangu kwa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini viongozi wake katika ngazi za chini kwa usimamizi wa miradi, fedha hizi tulizopewa zinafanya kazi ya ujenzi wa madarasa Nane, mabweni Matatu na Matundu 12 ya vyoo na mmejionea wenyewe waandishi jinsi kazi inavyo kwenda na kwa ubora unaotakiwa, pia tunatarajia majengo haya yote yakamilike kwa wakati uliopangwa,” alisema Jambeck.
Hata hivyo alisema kuwa, mradi huo umetoa ajira za muda kwa zaidi ya wananchi 300 ambao ni mafundi, vibarua na wapishi, huku baadhi ya wafanyabishara pia wananufaika na mradi huo kwa kuuza bidhaa kwa wafanyakazi, na vifaa vya ujenzi kwa mradi.
Sambamba na hayo aliishukuru Serikali kwani kuwatupatia shilingi milioni 100, ambazo wamejenga bwalo kubwa la kisasa ambalo litatumiwa na wanafunzi, hata hivyo alitoa rai kwa walimu, wazazi na wananchi kwa ujumla waendelee kuiamini Serikali yao pamoja na wao viongozi kwani wakishirikiana kwa pamoja kuisimamia miradi hii itakuwa bora zaidi na kudumu kwa muda mrefu, alisema Jambeck.