Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akisisitiza jambo wakati akikagua ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Milambo iliyopo Manispaa ya Tabora.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akiwasilisi kukagua moja ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Manispaa ya Tabora.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akimuelekeza jambo fundi mkuu wa mradi wa ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Msingi Matale, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akihimiza ukamilishaji wa mradi wa miundombinu ya elimu katika Shule ya Msingi Kiniga, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.
Mafundi wakiendelea na ujenzi miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Kazima iliyopo Halmashuri ya Manispaa ya Tabora.
Mafundi wakichanganya zege kwa ajili ya ujenzi miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Kazima iliyopo Halmashuri ya Manispaa ya Tabora.
Na: James Mwanamyoto – OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amewaelekeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanawasimamia mafundi kuongeza nguvu kazi itakayowezesha kukamilisha ujenzi wa miradi ya miundombinu katika shule za msingi na sekondari ili wanafunzi wanufaike na miundombinu hiyo.
Dkt. Msonde ametoa maelekezo hayo kwa nyakati tofauti akiwa wilayani Sikonge na Manispaa ya Tabora, mara baada ya kuhitimisha ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika halmashauri hizo.
Dkt. Msonde amewata viongozi hao kuhakikisha ndani ya siku mbili katika maeneo yote ambayo ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari unaendelea, kunakuwa na mafundi wa kutosha ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
“Nimetembelea ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari, hususani shule ya sekondari Kamagi na nimejionea ujenzi katika shule hiyo upo hatua ya msingi ambayo ina kwamisha lengo la Serikali,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde ameongeza kuwa, changamoto ya upungufu wa mafundi kama zilivyo nyinginezo inapaswa kutatuliwa na viongozi hao wa Sikonge na Manispaa ya Tabora kwani ni wajibu wao viongozi kuitatua o ili miradi ikamilike kwa wakati.
Dkt. Msonde amehimiza kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo ya elimu inapaswa kuwa ya kudumu ili itumiwe na vizazi vingi, hivyo Serikali haitarajii miundombinu hiyo ikikamiliza ichakae ndani ya muda mfupi na kuilazimu tena kutafuta fedha nyingine za kujenga miundombinu mipya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Bw. Selemani Pandawe amesema, yeye pamoja na watumishi anaowaongoza watajipanga kikamilifu kutekeleza maelekezo ya Dkt. Msonde ya kusimamia vema ujenzi wa miradi ya miundombinu ya elimu ili kuboresha utoaji wa elimu ya msingi na sekondari katika halmashauri yake.
Dkt. Msonde amekagua utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya elimu kwenye shule ya Sekondari Kamagi, Shule ya Sekondari Kiwere, Shule ya Msingi Matale na Kiniga zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ikiwa ni pamoja na Shule ya Msingi Mabatini, Shule ya Msingi Magereza na Shule za Sekondari za Milambo na Mabatini zilizopo Manispaa ya Tabora.