Mashujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Mzee Dominick Kijuu (mwenye kofia) aliyetoa eneo la ekari 4 kwa ajili ya kujenga shule eneo la Mtoo Kitongoji cha Mwembeni wilayani humo. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Serikali wa kitongoji hicho, Saluthary Naaly,Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Wallace Sichambo na Katibu wa Smaujata wa kata hiyo, Sarah Yohana.
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii
(SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani
Singida imeendelea kuwa moto wa kuotea mbali katika mapambano dhidi ya vitendo
vyote vya ukatili wa kijinsia ambapo ndani ya wiki moja wameweza kuwapata
mashujaa wapya 50 ambao wataongeza nguvu ya mapambano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Makamu
Mwenyekiti wa SMAUJATA Kata ya Manyoni, Wallace Shechambo alisema mashujaa hao
wapya wamepatikana kupitia kampeni yao ya Wawili kwa Wawili ‘ Two by Two ambayo
waliianzisha hivi karibuni na sasa inaonesha kupata mafanikio makubwa.
“Kampeni yetu ya ‘Two by Two’ imekuwa ya
mafanikio na nina amini hadi kufikia mwezi Septemba tutakuwa na mashujaa wapya
zaidi ya 150 ambao watatusaidia kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya vitendo
vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto,” alisema Shechambo.
Shechambo akizungumzia baadhi ya kazi
walizozifanya mwezi huu wa Juni, 2023 alisema walifanya kazi za usafi wa
mazingira katika kata hiyo kuzunguka viunga kadhaa vya mji wa Manyoni ikiwa ni
pamoja na mzunguko wa magari ‘Round About’ ya kutoka Itigi na Singida.
Alisema baada ya kufanya usafi huo viongozi wa
SMAUJATA walipata fursa ya kutoa elimu ya kuukataa ukatili kwa wananchi
walioshiriki kufanya usafi huo zoezi lililoongozwa na Afisa Afya wa Wilaya hiyo
Swedy Seif.
Shechambo katika mkutano huo alitoa elimu ya
uzalendo na namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili katika kata hiyo na
wilaya nzima ya Manyoni
Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Mwembeni
Saluthary Naaly akizungumza katika mkutano huo alipata fursa ya kutoa elimu
kuhusu ulinzi shirikishi ambao ni muhimu katika kukabiliana na vitendo vya
ukatili.
“Bila ya kuwa na ulinzi shirikishi
hatutaweza kukabiliana na vitendo vya ukatili niwaombe tuongeze nguvu katika
jambo hili hakika tutafanikiwa,” alisema Naaly.
Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa SMAUJATA wa
kata hiyo, Shujaa Neema Masabuni alitoa rai kwa walezi na wazazi kuwa makini
wanapozungumza mbele ya watoto hasa mambo ya ndani yanayohusu mahusiano au
kutoleana lugha za matusi wanapokuwa wamekoseana.
Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo Hussein Kheri
alitoa shukurani kwa wananchi walioshiriki katika zoezi hilo ambalo lilikuwa na
faida mbili ya kufanya usafi na kupata elimu yakupinga vitendo vya ukatili.
Mzee Mtundu ambaye ni mmoja wa mashujaa wa kata
hiyo aliwashauri wazazi na walezi kujenga urafiki na watoto wao jambo
litakalosaidia kujua changamoto walizonazo na kuwapatia msaada.
Mashujaa waliokuwa katika kampeni hiyo ni Afisa
Afya wa Wilaya ya Manyoni, Swedy Seif, Saluthary Naaly, Hussein Kheri, Joyce Peter, Neema Masabuni, Zena Salum, Mary
Vicent, Juma Mpangala, Mary Dominick, Wallace Shechambo, Mwalimu Juma Mtundu.
Katika tukio jingine mashujaa wote wa kata hiyo
wakiongozwa na viongozi wao walimpongeza Mzee Domonick Kijuu, Mzalendo wa ukweli
ambaye ameunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha
watoto wanapata mazingira mazuri ya kusomea ambaye ametoa eneo lake la ekari 4
bure kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya
Msingi eneo la Mtoo katika Kitongoji cha Mwembeni.
Wananchi wa kata hiyo pamoja na viongozi wa
SMAUJATA wakiongozwa na Mzee Kijuu (75)walikwenda kufanya usafi katika eneo
hilo ambapo Mwenyekiti wa Serikali wa Kitongoji
cha Mwembeni Saluthary Naaly alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi
umuhimu wa ujenzi wa shule katika eneo hilo kwani watoto wao wanao kadiriwa
kuwa ni zaidi ya 450 hutembea umbali mrefu wa kwenda kupata elimu Shule ya
Msingi Mwembeni na Manyoni huku wakipata adha kubwa wakati wa mvua za masika
kwa barabara kujaa maji na kuhatarisha maisha yao kutokana na mafuriko.
Mzee Kijuu akizungumza wakati wakifanya usafi
katika eneo hilo alisema amekuwa na furaha ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu
Hassan na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Mkoa wa Singida kwa kutoa eneo
hilo ambalo itajengwa shule kwa ajili ya kuwaandaa viongozi wa kesho.
“Nimelitoa eneo hili nililolitunza kwa muda
mrefu nikiwa na akili timamu kwa ajili ya kujenga shule itakayo waondolea adha
watoto kutembea umbali mrefu kwenda Shule ya Msingi Mwembeni na Manyoni kupata
elimu,” alisema Mzee Kijuu.
Wakizungumza katika eneo hilo wananchi waliofika
kufanya usafi wakiwa na wanafunzi wa darasa la tatu na sita wanaoishi nao,
walimshukuru mzee huyo kwa kutoa eneo na kupendekeza shule hiyo ikijengwa iitwe
Shule ya Msingi Kijuu ili kumuenzi.
Aidha, katika tukio lingine mashujaa wa kata hiyo
ya Manyoni walikwenda kwenye Kitongoji cha Tambukareli ambako walikuwa
wamealikwa kwenye mkutano wa hadhara na Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Aziza
Mbago kwa ajili ya kutoa elimu ya kupinga ukatili na kuzungumzia kampeni yao ya
‘Two by Two’.
Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Kata ya Manyoni
akizungumza katika mkutano huo aliwataka wananchi kuwa wazalendo na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo vimekithiri miongoni mwa jamii na kueleza kuwa moja ya njia ya kuvipunguza wazazi kuheshimiana, kuthaminiana na kunawajenga watoto kwa kuamini kuwa nyumbani kwao ni sehemu sahihi ya kuishi badala ya kuwaacha wakitangatanga mitaani.
Shujaa Henry Mallya akizungumzia wazazi
waliotengana alisema ni muhimu kujua mazingira alipo mzazi mwenzie ili waweze
kusaidia katika malezi ya watoto au hata kumpata pale mmoja kati yao atakaposhindwa kutimiza
wajibu wake wa matunzo kwa familia husika jambo litakalo punguza kuwepo kwa
watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.
Kwa upande wake Katibu wa SMAUJATA Kata ya Manyoni,
Sarah Yohana alizungumzia wajibu wa
wazazi wote wawili katika malezi ya watoto wao.
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Tambukareli
Shujaa Aziza Mbogo alisema kampeni ya ‘Two by Two’ ndio mkombozi katika
kutokomeza ukatili katika wilaya hiyo.
Mashujaa wa SMAUJATA waliohudhuria mkutano huo
katika Kitongoji hicho cha Tambukareli uliokuwa na wananchi zaidi ya 100 ni
Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Kata ya Manyoni, Wallace Shechambo, Katibu, Sarah
Yohana, Mtunza Hazina, Joyce Peter
Mratibu wa SMAUJATA, Zena Salumu, Mshauri wa SMAUJATA, Henry Mallya na
Matilda