Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge (mwenye miwani) akimkabidhi vifaa hivyo Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Bi. Lydia Nzema.
NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID.
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umekabidhi vifaa tiba kwenye Hospitali
ya Rufaa ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho
ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo huadhimishwa Juni 23 kila mwaka kwania ya
kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika Maendeleo ya bara la Afrika.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi
msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge alisema
Hospitali na watoa huduma za afya ni wadau
muhimu nan i kiungo baina ya Mfuko na wahanga wanaopata magonjwa au ajali
zinazotokana na kazi na jukumu kubwa la WCF ni kutoa fidia pale mfanyakazi
anapoumia au kuugua kutokana na kazi hivyo msaada huo ni kutambua mchango wa
watumishi wa umma katika kuhudumia wananchi na Mfuko unaamini msaada huo
utarahisisha utendaji wao wa kazi na hivyo kuleta tija katika sekta ya afya.
“Watumishi ni sehemu ya umma na WCF ni sehemu
ya umma kwa sababu inatoa fidia kwa wafanyakazi, na ninyi mnahudumia jamii,
tunajua mnatoa huduma nzuri, lakini tukiwaunga mkono kwa kutoa vifaa zaidi mtatoa
huduma zenu kwa ubora zaidi na wagonjwa mnaowahudumia watapona haraka na
kurejea katika uzalishaji na hivyo kujenga uchumi wa taifa.” Alifafanua.
Bi. Laura aliipongeza serikali ya awamu ya
sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha huduma za afya nchini ambapo inashuhudiwa
ongezeko kubwa la miundombinu ya afya katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya Rufaa
Mwananyamala, Bi. Lydia Nzema aliishukuru WCF kwa msaada huo wa vifaa tiba
ambavyo alisema vitasaidia kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.
“Hospitali hii ni ya umma inahudumia jamii
yote iliyo katika eneo hili, na tunahudumia watu wengi vifaa hivi vitarahisisha
na kupanua wigo wa wagonjwa tunaowahudumia kwani uhitaji ni mkubwa sana.”
Alifafanua.
Aidha kwa upande wao Maafisa Wafawidhi Kanda,
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kutoka Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini na
Kanda wa ziwa, wametoa wito kwa waajiri kujisajili na Mfuko ili kuwawezesha
watumishi wao kuwa na uhakika wa kipato pindi wanapopatwa na majanga wawapo
kazini.
“Tunapenda kuwakumbusha watumishi wa umma
Tanzania bara kuzingatia miongozo ya usalama na afya amahli pa kazi, lakini
inapotokea bahati mbaya mtumishi amepata changamoto ya ajali kazini au ugonjwa
afike ofisi za WCF ili aweze kupata hakiz ake kama mtumishi.” Alisema Nuru
Ashraf, Afisa Mfawidhi WCF, Kanda ya Kati.
Naye Rose Satta, Afisa Mfawidhi Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini, alisema katika maadhimisho hayo wameendelea kutoa elimu
na kuwahudumia waajiri na watumishi mbapo alisema Mfuko umerahisisha sana utoaji
wa huduma kwa njia ya kidijitali hivyo watumie huduma hiyo kutoa taarifa za
matukio ya ajali, magonjwa au kifo kwani itarahisisha Mfuko kuchataka madai yao
kwa haraka.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge (mwenye miwani) akimkabidhi vifaa hivyo Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Bi. Lydia Nzema.
Baadhi ya Wafanyakazi wa WCF na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala wakiwa katika picha pamoja na vifaa hivyo.
Afisa Mfawidhi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Rose Satta (kushoto) akimuhudumia mteja kwenye ofisi za WCF, jijini Mbeya.