Na Victor Masangu,Kibaha
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakar Kunenge amewataka viongozi wa halmashauri ya mji Kibaha licha ya kupata hati ya ukaguzi iliyoridhisha (Hati safi) wasibweteke na badala yake wanapaswa kutatua kero na changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Kunenge ametoa kauli hiyo wakati wa Baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya Kibaha mji lilioandaliwa kwa ajili ya kujadili taarifa ya utekelezaji wa hoja ya ukaguzi na taarifa ya hati ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Katika kikao hicho ambacho kilihudhuliwa na na viongozi mbali mbali wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) wakuu wa idara,watendaji kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa,wakaguzi wa hesabu,pamoja na Mkuu wa Mkoa ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.
Kunenge alisema kuwa upatikanaji wa kupata hati safi ni hatua nzuri lakini inapaswa iendane na kwenda sambamba na kuwahudumia wananchi kwa vitendo katika Mambo mbali mbali ikiwemo upatikanaji wa huduma ya maji safi na salamà,kuboresha hali ya elimu,afya pamoja na maeneo mengine ili kulete tija zaidi.
“Nimeona taarifa yenu ya kupata hati safi katika halmashauri ya mji kibaha,mimi nawapongeza sana kwa hatua hii lakini hatuwezi kufurahia kupata tu hati safi wakati wananchi wetu katika maeneo mbali mbali bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ni vema viongozi na watendaji tufurahie kupata hati lakini tutatue na kero za wananchi wetu waweze kupata huduma zinazostahili,”alisema Kunenge.
Kadhalika aliwawataka viongozi wote wa halmashauri kuweka mipango mikakati mizuri ambayo itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kujibu hoja zote zilizotolewa katika taarifa ya utekelezaji ili kuweza kuzifunga kwa wakati ili kuondokana na dosari zilikuwepo.
Aliongeza kwamba lengo lake kubwa ni kuendelea kushirikiana bega kwa bega na viongozi wote katika ngazi zote kwa lengo la kuweza kuufanya Mkoa wa Pwani uweze kuendekea kuwa kinara zaidi katika suala zima la uwekezaji wa ujenzi wa viwanda na kwamba kunatakiwa kuachana kabisa na kuwepo kwa migogoro ya ardhi.
“Hivi karibuni Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan alitupongeza kwa dhati katika Mkoa wetu wa Pwani kuwa kinara katika uwekezaji wa viwanda kwa hiyo sisi tunapaswa kuweka mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji ikiwemo kuhakikisha tunatatua migogoro ya ardhi katika maeneo yetu,”alisema Kunenge.
Awali kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha mji Mhandisi Mshamu Munde alibainisha kwamba kwa kipindi kinachoishia juni mwaka 2021 halmashauri ilikuwa na mapendejezo ya hoja zipatazo 39.
Pia alibainisha kuwa taarifa ya hati ya ukaguzi wa hesabu za halmashauri kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 imeweza kupata hati inayoridhisha (hati safi) ambayo imetokana baada ya kufanyiwa ukaguzi wa kina katika maeneo mbali mbali.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mji Mwajuma Nyamka aliipongeza halmashauri hiyo kwa kufanikiwa kupata hati safi mfululizo na kuwahimiza viongozi licha ya kupata hati hiyo wasikilize changamoto zinazowakabili wananchi ili waweze kuzitafutia ufumbuzi katka sekta tofauti.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Kibaha Mussa Ndomba alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ushauri na kuahidi kuyayanyia kazi maelekezo na maagizo yote yaliyotolewa kwa ajili ya Kuhakikisha baadhi ya hoja zinafanyiwa kazi mapema na ili ziweze kufungwa.
Halmashauri ya mji Kibaha iliyopo Mkoa wa Pwani imeweza kufanikiwa kupata hati inayoridhisha (Hati safi) kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi ya hesabu kutolewa.