Waziri wa Kazi,Ajira,Vijana na wenye ulemavu Prof .Joyce Ndalichako akizungumza katika semina hiyo jijini Arusha.
Mtendaji Mkuu wa TPSF,Raphael Maganga akizungumza katika semina hiyo jijini Arusha
Picha ya Waongoza watalii kutoka kanda ya kaskazini wakifuatilia semina hiyo iliyofanyika jijini Arusha
Julieth Laizer,Arusha .
Waziri wa Kazi,Ajira,Vijana na wenye ulemavu,Profesa Joyce Ndalichako amewataka waongoza watalii nchini kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza vivutio vya utalii sambamba na kuwapeleka watalii kujionea vivutio hivyo ili kuweza kufurahia neema ya kipekee iliyopo katika nchi yetu.
Hayo yamesemwa jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya kukuza ujuzi kwa waongoza watalii yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kazi,Ajira,vijana na wenye ulemavu kwa kushirikiana na TTGA yaliyofanyika kwa muda wa siku sita jijini Arusha.
Ndalichako amesema kuwa,ni jukumu la waongoza watalii kuhakikisha wanatangaza vivutio hivyo kwa wageni mbalimbali wanaofika nchini ili kuongeza idadi ya watalii watakaotembelea vivutio hivyo kwa wingi na hatimaye kuongeza pato la Taifa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TPSF ,Raphael Maganga amesema kuwa utoaji mafunzo hayo kwa waongoza watalii hao utasaidia sana kuwa mabalozi wazuri katika utendaji kazi wao na kuongeza idadi ya watalii na kuweza kufikia malengo yaliyowekwa .
Maganga amesema kuwa,sekta ya utalii inaendelea kukua sana na inaendelea kuajiri zaidi ya watanzania 1.5 milioni ikiwa ni sekta inayoajiri watanzania wengi sana.
“Taasisi ya sekta binafsi Tanzania (TPSF) tunaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha makampuni ambayo hayatoi mikataba yanafuatiliwa ili watu waweze kupata haki zao za msingi. “amesema.
Mwenyekiti wa chama cha waongoza watalii Tanzania (TTGA) ,Lembris Loipuko amesema kuwa, jumla ya waongoza watalii 696 kutoka kanda ya kaskazini wameweza kupata mafunzo hayo ambapo mada mbalimbali zimetolewa ikiwemo huduma kwa wateja,huduma ya kwanza ya kisasa,Utangulizi wa huduma ya uongozi wa watalii Uwandani .
Amesema kuwa,kupitia mafunzo hayo wataweza kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza ili kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza utalii nchini pamoja na juhudi za serikali za kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025.
Aidha amesema kuwa,pamoja na mafanikio mbalimbali ,wameomba serikali iwasaidie kuwa na vifurushi rafiki kwa waongoza watalii,kwani wanasikitishwa sana na serikali kusitisha huduma na kukataa kuhuisha vifurushi vya Bima ya Afya kupitia NHIF ambavyo waongoza watalii walikuwa wanufaika.
Aidha waliomba serikali kuwapatia gari la kutoa msaada kwani kwa upande wa mlima Kilimanjaro halipatikani kwa wakati jambo linalopelekea kuhatarisha maisha ya wageni na wapanda mlima kwa ujumla.