Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023 Abdallah Shahib Kaim amepongeza Uongozi wa Wilaya ya Same wakiongozwa na mkuu wa Wilaya hiyo Kasilda Mgeni kwa usimamizi mzuri wa Miradi inayotekelezwa katika eneo hilo.
Ametoa pongezi hizo baada ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kuwasili Mkoa wa Kilimanjaro na kuanza mbio zake kuona, kuweka Mawe ya Msingi na kukagua miradi mbalimbali.
Kiongozi huyo amesema katika Miradi yote Saba iliyopitiwa, Mwenge wa Uhuru umefanya ukaguzi wa kina kujiridhisha na ubora na viwango vinavyo hitajika, ukaguzi wa Nyaraka na viambatanishi muhimu, pia muongozo mbalimbali Katika utekelezaji wa Miradi ya serikali na kujiridhisha hakuna dosari yoyote, akisema mafanikio hayo ni usimamizi mzuri wa viongozi waliopewa jukumu la kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali yake katika kuboresha huduma.
Miongoni mwa Miradi hiyo iliyopitiwa ni ukarabati wa kiwango cha Zege Mita 810 za eneo korofi katika Barabara ya Hedaru-Vunta-Myamba, mradi unaotekelezwa na Wakala WA barabara Mijini na Vijijini TARURA Wilaya ya Same.
Awali akitoa taarifa ya Ujenzi wa Maeneo hayo korofi Meneja wa TARURA Wilaya ya Same Mhandisi James Mnene alisema ujenzi wa maeneo korofi ya Barabara ya Hedaru-Vunta-Myamba yenye urefu wa Mita 810 utagharimu takribani shilingi Milioni 655.5 na utamilika katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2022-2023.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni, Mkuu wa wilaya Hai Amir Mkanipa alisema ukarabati unaofanyika pamoja na kuboresha huduma utaongezeko mapato ya Halmashauri kwa wafanyabiashara kupata urahisi wa kusafirisha mizigo.
Mbunge wa Jimbo la Same Masharik Anna kilango Akizungumza kwa niaba ya wananchi amemshukuru Serikali ya Rais wa awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuwakomboa wananchi wa Vuntaa Mamba Myamba kwa kuleta Fedha nyingi kukamilisha Miradi mikubwa, pia juhudi za viongozi wakiongozea na Mkuu wa wilaya hiyo ya Same Kasilda Mgeni kwa usimamizi kuhakikisha Miradi inatekelezwa kama ilivyo pangwa.
Katika Wilaya ya Same Mwenge wa Uhuru umepitia jumla ya Miradi Saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilion 3.6, Miradi mingine iliyotembelewa ni Miradi ya Maji, Afya na Elimu.