MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu, akichangia bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 leo Juni 21,2023 bungeni jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amesisitiza kuwa dhamira ya serikali kuongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es salaam kupitia Kampuni ya DP World ya Dubai ni njema na wala serikali haina mpango wa kuiuza bandari hiyo.
Aidha,ametaja makundi manne yanayokwamisha hatua hiyo ikiwemo wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wamekuwa wanaingilia mchakato huo ili wao waendelee kufaidika na udhaifu wa bandari.
Mtaturu amesema hayo Juni 21,Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia bajeti ya serikali yam waka wa fedha wa 2023/2024.
Mtaturu amesema dhamira ya serikali ya kumuweka mwekezaji ni njema na kama Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu analiunga mkono.
“Mimi ni mjumbe wa kamati ya miundombinu,nimekuwa nikiongea mara tatu hapa katika suala la bandari ,jamani bandari ndio kioo chetu ,kumekuwa na kauli mbalimbali zinatolewa lakini nimpongeze Mh Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ametoa kauli nzuri sana kuhusiana na bandari ,niseme mawazo tutaendelea kuyachukua ila kusiwe na upotoshaji, sisi hatutarudi nyuma, tunataka tuwekeze tuongeze pato la Taifa ,”amesisitiza.
Ametaja makundi hayo kuwa ni suala la wapinzani kutaka kutuzuia tusiendelee , baadhi ya wafanyakazi wa TPA na TRA wanaofaidika na mfumo huu mbaya wa kuendesha bandari yetu nan ne ni bandari shindani zilizopo kwenye ukanda huu ambazo hazipendi sisi tufanikiwe,
Amesema kampuni ya DP World ina uwezo mkubwa sana na kusisitiza kwamba kama nchi haitauza bandari kwak uwa ni mali ya watanzania.
“Mh Rais ameshasema tuwaondolee hofu kwa sababu hatuna sababu ya kuogopa lakini hofu ipo,tulikuwa na stendi yetu pale Mnazi Mmoja Kisutu,wananchi waliandamana kwa sababu inapelekwa Ubungo, wakasema ni mbali sana,leo tunavyoongea stendi ipo Mbezi ,mi niwaombe wananchi waondoe hofu,nia yetu ni njema ,tuendelee kuiunga mkono serikali ili iongeze mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi,”amesisitiza.