Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dk.Dorothy Gwajima (katikati) akiwakabidhi cheti cha heshima viongozi wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Mkoa wa Singida kwa kufanikiwa katika mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto. Kutoka kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Smaujata Wilaya ya Manyoni, Tatu Ramadhani, Makamu Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Singida, Ambwene Kajula, Mwenyekiti wa Smaujata, Wilaya ya Manyoni, Juma Amrani na Mwenyekiti wa Smaujata, Wilaya ya Itigi, Hadija Kaherewa.
Na Dotto Mwaibale, Dodoma
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu imetoa
cheti cha heshima cha pongezi kwa Shujaa na Maendeleo ya Jamii Tanzania (SMAUJATA)
Mkoa wa Singida kutokana na kufanikiwa katika mapambano dhidi ya ukatili kwa
watoto.
SMAUJATA Mkoa wa Singida imepewa cheti hicho katika kilele cha Siku ya
Mtoto wa Afrika kilichofanyika Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa wizara
hiyo, Dk. Dorothy Gwajima ambaye alimkabidhi Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa
wa Singida, Ambwene Kajula.
Akizungumza wakati akikabidhi cheti hicho, Dk. Gwajima
aliwashukuru wanasmaujata wote nchi nzima kwa mchango wao mkubwa walioufanya
katika kuwatetea watoto ambapo alitumia nafasi hiyo kuyaomba mashirika
mbalimbali na watumishi wa Serikali na wizara kwa ujumla kuwatumia
wanasmaujata katika kufanya kazi za jamii hasa zinazowahusu watoto kwani tayari
wameonesha umahiri na uaminifu katika suala zima la kupinga ukatili dhidi ya
watoto.
Aidha, Gwajima aliwataka Smaujata wote nchini kuendelea kufanya
kazi kwa bidii na kwa weledi na kuwa tuzo za Smaujata Day bado zipo zitatolewa
wakati wa kampeni ya wiki mbili ya kupinga ukatili wa kijinsia itakayofanyika baadae.
Naye Mwenyekiti wa Smaujata Taifa, Sospeter Bulugu, aliwataka
wanasmaujata kuendelea kushikamana na kwamba kwa sasa wako kwenye mchakato wa
kuanzisha jumuiya ambayo itasaidia kuwaweka pamoja na kujitanua zaidi katika shughuli
zao.
Pia Bulugu aliwataka wanasmaujata kurejea kwenye malengo yao
kwani kupinga ukatili ni moja ya kipengele kidogo kati ya mambo mengi
waliyonayo na akatumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kujiunga na Smaujata
kwani ni ya watanzania wote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa Singida, Shujaa Dismas Kombe ameishukuru Wizara
ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu kwa kutambua mchango mkubwa
wa Smaujata mkoani hapa katika mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto na kuamua
kuwatunuku cheti hicho cha heshima.
“ Heshima hii pamoja na pongezi hizi
ziwafikie mashujaa na wadau wote katika mkoa wetu wakiwemo maafisa ustawi wa viongozi
wa dini,walimu, viongozi wa chama na Serikali
ambao kwa namna moja ama nyingine wameshirikiana na SMAUJATA katika
mapambano haya ya ukatili dhidi ya watoto,” alisema Kombe.
Alisema cheti hicho walichotunukiwa kitakuwa chachu ya kuongeza mapambano
dhidi ya vitendo hivyo ambavyo vimekithiri katika maeneo mengi na kuwa
ushirikiano baina yao ndio njia pekee itakayosaidia kuutokomeza ukatili huo
katika jamii.
Katika kilele hicho cha Siku ya Mtoto wa Afrika Mwasisi wa kaulimbiu ya kupinga ukatili Kitaifa ya ‘Don’t Touch’ ambaye alipongezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kupinga ukatili, Mkaguzi wa Polisi, Francis Msuku kutoka Kata ya Gambushi mkoani Simiyu, Bariadi alikuwa kivutio huku kila mshiriki wa siku hiyo akitaka kuzungumza na kupiga picha naye,
Kutokana na kazi nzuri iliyotukuka anayoifanya ya mapambano ya ukatili katika kata hiyo Machifu na Viongozi wa Utamaduni walifurahishwa na utendaji kazi wa Polisi Jamii chini ya uongozi wake na kufikia hatua ya kumtunuku heshima ya kuwa chifu kutokana na kukomesha vitendo vyote vya ukatili ndani ya kata hiyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dk.Dorothy Gwajima,akimkabidhi cheti cha heshima, Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa, Sospeter Mlugu katika hafla hiyo.