Na Mwandishi wetu, Babati
BAADHI ya Madiwani wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara wamemshukuru na kumpongeza Mbunge wa viti maaluma wa mkoa huo Regina Ndege kwa kuwasafirisha na wajumbe wa mkutano wa UWT wa Mkoa huo kwenda jijini Dodoma Bungeni kwenye ziara ya mafunzo na utalii.
Waliosarifi kwenda Dodoma ni madiwani wa viti maalum, wenyeviti, makatibu wa Wilaya na Kata wa jumuiya ya umoja wa wanawake (UWT) na wajumbe wa UWT wa wilaya na wadiwani wa kata wanawake wa Kata.
Mmoja kati ya diwani wa viti maalum wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Esta Joel amemshukuru mbunge huyo Regina Ndege kwa kufanikisha ziara yao ya kutembelea jijini Dodoma ili kujifunza.
“Tunamshukuru Mbunge wetu wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Regina Ndege kwa kutualika jijini Dodoma ambapo tumejifunza mengi kwa kutembelea Bungeni na kufika ukumbi wa Jakaya Kikwete zilipo ofisi za CCM Taifa,” amesema Esta.
Amesema kwenye wilaya ya Mbulu kuna wajumbe 91 ila wajumbe 80 ndiyo walihudhuria kutoka kata mbalimbali na wajumbe wawili wa mkoa Mary Margwe na Grace Qwintini na wengine walikuwa wagonjwa na wazazi waliojifungua watoto hawakwenda Dodoma.
“Pamoja naye tunawashukuru wabunge wote wa mkoa wa Manyara kwa kutuonyesha ukarimu wao tukiwa Dodoma hadi tulipofika kwa mwenyeji wetu mhe Regina Ndege,” amesema Esta.
Amesema wataendelea kushirikiana na mbunge huyo katika shughuli mbalimbali za kijamii kwani amewaonyesha ukarimu mkubwa wakiwa jijini Dodoma kwenye ziara hiyo.
Diwani wa viti maalum wa halmashauri ya mji wa Babati, Aziza Kambi amemshukuru mbunge huyo Regina Ndege kwa kuwaalika wao wakiwa na wajumbe wenzake 24 kutoka halmashauri ya mji wa Babati na wajumbe 63 wa halmashauri ya wilaya ya Babati.
Kambi amesema kupitia mwaliko huo wa mbunge huyo wamejifunza namna ambavyo wabunge wanavyoendesha shughuli zao wakiwa Bungeni ikiwemo maswali yanavyoulizwa hivyo madiwani wamepata elimu nzuri.
“Kwa kweli tunamshukuru mbunge wetu wa viti maalum wa mkoa wa Manyara kwa kutupa mwaliko wa kuja Dodoma kwenye ziara ya kujifunza na kutalii pia,” amesema diwani Kambi.
Mbunge Regina Ndege ambaye kitaaluma ni mwalimu, awali pia aliwahi kushika nafasi ya Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana (UVCCM) wa Mkoa wa Manyara.