Meneja wa Benki ya Nmb Tawi la Namtumbo mkoani Ruvuma Atu Mwanjejele akizungumza wakati wa droo ya washindi wa kampeni ya Bonge la mpango mchongo wa kilimo awamu ya pili kanda ya Kusini ambapo wakulima watano walijinyakulia zawadi ya fedha taslimu Sh.100,000 na Chama cha Msingi cha Ushirika Lwinga kilishinda Pikipiki,katikati mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Mryangi Kuruchumira na kulia kaimu meneja wa Nmb kanda ya kusini Roman Degeleki.
Meneja wa Benki ya Nmb Tawi la Namtumbo mkoani Ruvuma Atu Mwanjejele kushoto na Mfanyakazi wa Nmb kanda ya kusini Robert Samji wakimpa zawadi ya T-shirt mmoja wa wateja wa Benki hiyo jana.
Mwandishi Mkuu wa Chama cha Msingi cha Ushirika Lwinga Ushuru(Lwinga Amcos) Hamidu Komba akijaribu kuwasha Pikipiki ambayo Chama hicho kimeshinda katika droo ya Bonge la mpango mchongo wa kilimo awamu ya pili kanda ya Kusini iliyofanyika katika viwanja vya soko kuu la Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mwandishi Mkuu wa Chama cha msingi cha Ushirika wa Lwinga Amcos Hamidu Komba, akizungumza baada ya Chama hicho kujinyakulia zawadi ya Pikipiki katika droo ya Bonge la mpango mchongo wa kilimo awamu ya pili kanda ya kusini iliyoendeshwa na Benki ya Nmb.
Kaimu meneja wa Benki ya Nmb kanda ya kusini Roman Degeleki akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Bonge la mpango mchongo wa kilimo awamu ya pili kanda ya kusini iliyozinduliwa na Benki hiyo jana,katikati mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Namtumbo Mryangi Kuruchumira na meneja wa Benki hiyo Tawi la Namtumbo Atu Mwanjejele.
Kaimu meneja wa Nmb kanda ya kusini Roman Degeleki na meneja wa tawi la Namtumbo Atu Mwanjejele kushoto na Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Mryangi Kuruchumira aliyevaa shati jeupe wakipeperusha Bendera kama ishara ya uzinduzi rasmi wa kampeni ya Bonge la mpango mchongo wa kilimo awamu ya pili kanda ya kusini katika viwanja vya soko kuu mjini Namtumbo.
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
BENKI ya NMB, imezindua kampeni ya Bonge la Mpango Mchongo wa kilimo kanda ya Kusini ambapo wakulima watano wameshinda zawadi ya fedha taslimu na Chama kimoja cha Msingi(Amcos)wilayani Namtumbo kimeshinda zawadi ya Pikipiki.
Uzinduzi huo katika kanda ya Kusini umefanyika jana katika viwanja vya soko kuu mjini Namtumbo, na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi wakiwemo wakulima na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika wilayani humo.
Mwakilishi wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini Roman Degeleki alisema,Benki imeamua kuzindua kampeni ya Bonge la mpango mchongo wa kilimo awamu ya pili kanda ya kusini ambapo Amcos na wakulima watakaoweka akiba kupitia Benki hiyo wataingia kwenye orodha ya wanaostahili kushinda zawadi mbalimbali.
Alisema,lengo la kampeni hiyo ni kurejesha faida kwa wateja pamoja na kuhamasisha Watanzania kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba kwani bado Benki ya NMB inaendelea kutoa mamilioni ya fedha.
Aliongeza kuwa,NMB imetoa upendeleo mkubwa hasa kwa mkulima mmoja mmoja na wale waliojiunga kwenye vyama vya msingi vya Ushirika(AMCOS)ambao wataendelea kupata zawadi ya fedha na vyombo vya usafiri zikiwemo pikipiki,guta ili ziweze kusaidia katika shughuli zao za uzalishaji mali.
Alisema,kupitia mpango huo zaidi ya Sh.milioni 40 zitatolewa kama zawadi kwa washindi na kampeni hiyo itaendeshwa ndani ya wiki tano na kila wiki wakulima watano watapokea fedha kiasi cha Sh.100,000 kila mmoja huku Amcos itakayoibuka mshindi itapata Pikipiki.
Degeleki amewataja wakulima walioshinda Sh.100,000 kila mmoja kwenye droo ya wiki hii ni Alex Nombo wa Litembo Mbinga,Melina Saanze wa Mtwara,Malongo James wa Songea,Mustapha Milanzi wa Nanyumbu mkoani Mtwara na Hamidu Omary wa Mtwara.
Pia alikitaja Chama cha Msingi cha Ushirika kilichojinyakulia Pikipiki kwenye mchongo wa kilimo kuwa ni Lwinga Amcos ya mjini Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya,ameishukuru Benki hiyo kwa kuwakumbusha Watanzania kuhusu kujiwekea akiba kupitia akaunti kwani suala la kuweka akiba ni jambo muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku.
Alisema,kila siku yanaibuka matatizo ya dharura ambayo yanahitaji kutumia fedha nyingi na kama hauna akiba unaweza kupata wakati mgumu,lakini ukiweka akiba kwenye akaunti yako unaweza kutatua na kumaliza shida yako kwa urahisi na haraka sana.
Ngollo ametoa wito kwa Watanzania hususani wakazi wa wilaya ya Namtumbo,kutumia fursa hiyo iliyoletwa kwa manufaa yao na fedha watakazoweka zinabaki kuwa zao na wala siyo za Nmb.
Ameipongeza Benki ya Nmb kutoa zawadi hizo kwani zitasaidia kwa vyama vya msingi vya ushirika ambavyo vina changamoto nyingi kwenye uendeshaji ikiwemo usafiri katika kutekeleza majukumu na kusafirisha mizigo.