Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – Mhe. Hemed Suleiman Abdullah akiwa katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar – Mhe. Zubeir Ali Maulid na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi – Idrisa Mustafa (kushoto) wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 25 ya Benki ya NMB iliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip tawi la Aiport – Visiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB Dkt. Edwin Mhede pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna wakimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – Mhe. Hemed Suleiman Abdullah medali kumvisha Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar – Mhe. Zubeir Ali Maulid kwa kuongoza bonanza la ‘NMB Vita Nikuvute’ lilioandaliwa na Benki ya NMB kwa ajili ya kusherehekea safari ya mafanikio ya miaka 25 visiwani Zanzibar. Akishuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi – Idrisa Mustafa .
Uongozi wa Benki ya NMB katika picha ya pamoja wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 25 ya Benki hiyo, iliyofanyika katika hoteli ya Golden Tulip tawi la Aiport – Visiwani Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeipongeza Benki ya NMB kwa safari yake ya mafanikio yaliyotukuka ya miaka 25! Haya yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar – Mhe. Hemed Suleiman Abdullah, wakati wa sherehe ya maadhimisho ya miaka 25 ya benki hiyo iliyofanyika visiwani Zanzibar.
Mhe. Hemed alibainisha kuwa Serikali inaheshimu, inajali na kuthamini mchango endelevu wa taasisi hiyo kubwa na kiongozi hapa nchini, katika kustawisha Sekta za kimkakati visiwani humo, hasa za elimu, afya, utalii na uvuvi.
Aidha,alielizea kuwa wanajivunia sana ushiriki na mchango wa NMB katika maendeleo ya Zanzibar, huku akifafanua kuwa benki hiyo imeweka msukumo mkubwa katika kuchagiza ustawi wa maendeleo ya Wazanzibari, huku akiitabiria mafanikio makubwa zaidi kitaifa na kimataifa.
“Niwahakikishie tu kwamba NMB mtapata mafanikio makubwa mno, kwani mmekuwa vinara wa kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii, mchango wenu kwa jamii ya watu wa chini kabisa ni mkubwa na sishangai wala kujiuliza ukubwa wa mapato na faida yenu unatokana na nini, siri ya mafanikio yenu ni kujali jamii inayowazunguka”.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alikiri kufurahishwa na ushirikiano mkubwa inaopata benki yake kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar, huku akiahidi kudumisha ushirikiano huo.
Bi. Ruth aliieleza kuwa, wanajisikia fahari Zanzibar kuwa katika safari yao ya mafanikio kwa miaka 25 tangu NMB ilipo binafsishwa mwaka 1997, kwani safari haijakuwa rahisi kihivyo.
“Ilikuwa ni safari ngumu, tuliyoianza na matawi 97 tu huku huduma karibu zote zikipatikana matawini tu, lakini sasa tuna matawi 229, ATM na mawakala Zaidi ya 20,000, pamoja na mifumo ya kidijitali inayowezesha kupata kila huduma nje ya matawi, ikiwamo kufungua akaunti na kukopa ‘Mshiko Fasta’ bila dhamana yoyote.
Benki ya NMB ina matawi matatu Zanzaibar na mwaka huu kabla haujaisha wameahidi kufungua mengine matatu huko Nungwi, Paje na kwingineko iki kuendelea kutoa huduma za kibenki wa watu wengi visiwani humo.
Tayari NMB ina ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (E GAZ) ya kutoa suluhishi za malipo na makusanyo kwa taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wanashirikiana pia na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), kutengeneza mifumo ya kufuatilia taarifa na kuhudumia wawekezaji, pamoja makubaliano na Mamlaka ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe katika kuhifadhi Bustani ya Forodhani ambayo ni moja ya vivutio vya kitalii.
Tunaitakia Benki ya NMB, maadhimisho mema ya miaka 25!