Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umewataka wakazi wa Shinyanga na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kujisajili na kupatiwa cheti cha kuzaliwa katika kipindi hiki cha kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea Mkoani humo kwani ni fursa ya kipekee ambapo huduma hiyo imesogezwa kwao ili kuwafikia wengi kwa urahisi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari , Afisa habari wa RITA Bw. Goodluck Malekela amesema kuwa RITA imejipanga vizuri kuhakikisha inaendelea kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani.
“RITA imejipanga vizuri kuhakikisha inaendelea kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani, ni vyema wakachangamkia fursa hii na kuja kwa wingi kusajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa kwani Vyeti hivyo vina umuhimu mkubwa na vitawasaidia kwenye mambo mengi ikiwemo Ajira, Elimu hata kupata kitambulisho cha Uraia”,amesema Malekela.
Ameongeza kuwa mbali ya kusajili na kutoa Vyeti vya Kuzaliwa hapo hapo ndani ya siku moja timu ya RITA imejipanga kutoa elimu ya Mirathi, kuandika na kuhifadhi Wosia ili kuondoa wimbi kubwa la imani potofu kwa watu wenye kuamini Wosia ni Uchuro.
Hata hivyo wananchi mbalimbali wameendelea kujitokeza kusajiliwa na kuchukua vyeti vyao huku wakiipongeza Serikali kuanzisha kampeni hii inayosaidia huduma kuwafikia kwa ukaribu na kwa urahisi bila usumbufu.
“Serikali imefanya jambo jema sana kuanzisha hili zoezi,nilisikia Tangazo nikaja jana na kweli leo nimepata cheti changu cha kuzaliwa siku moja baada ya kujiandikishala,RITA wanafanya kazi nzuri na wametuhudumia vizuri”,amesema Shija Kulwa mkazi wa Old Shinyanga aliyepatiwa Huduma.
RITA imeweka kambi ya siku kumi mkoani Shinyanga kwenye viwanja vya Saba saba Manispaa ya Shinyanga kuanzia Juni 11, 2023 mpaka tarehe 20 Juni 2023 ikiendelea kutoa huduma ya Usajili vyeti vya kuzaliwa na kutoa Elimu juu ya mirathi , kuandika na kuhifadhi wosia.
Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria inayojulikana “Mama Samia Legal Aid Campaign” inayotokana na azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba msaada wa kisheria unatolewa kwa wananchi wote ili kupata haki, usawa, amani na maendeleo imezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme Jumapili Juni 11, 2023 katika uwanja wa Sabasaba Mjini Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme (wa pili kulia) akizindua Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria inayojulikana “Mama Samia Legal Aid Campaign” Jumapili Juni 11,2023 katika Uwanja wa Sabasaba Mjini Shinyanga. Wa kwanza Kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mhe. Santiel Kirumba akifuatiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul. Kulia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Donald Magesa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme (wa pili kulia) akizindua Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria inayojulikana “Mama Samia Legal Aid Campaign” Jumapili Juni 11,2023 katika Uwanja wa Sabasaba Mjini Shinyanga.
Banda la RITA