Afisa Uhusiano kutoka GGML, Ruth Mharagi akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya sekondari wasichana Nyankumbu, namna ya kutumia pedi pindi wawapo kwenye hedhi.
NA MWANDISHI WETU
Hedhi ni sehemu ya maisha ya kawaida na yenye afya, lakini kwa watu wengi wanaopata hedhi, ni chanzo cha aibu, hofu na ubaguzi. Ukosefu wa upatikanaji wa bidhaa za kutosha za hedhi safi na salama na elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana na hata wazazi, inaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya binti, elimu yake na hata maisha yake.
Kiujumla afya duni ya hedhi na usafi hudhoofisha haki za kimsingi ikiwa ni pamoja na haki ya kufanya kazi, kwenda shule kwa wanawake, wasichana na watu wanaopata hedhi hali hii inazidisha ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi.
Ni kwa sababu hiyo kwamba kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), inayothamini maendeleo endelevu kwa jamii, inachukua hatua kusaidia mipango ya hedhi safi na salama katika jamii inayozunguka migodi yake.
Akizungumzia jitihada za kampuni hiyo katika kujali na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa pedi kwa wasichana, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti-GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo anasema GGML inaamini kwamba kwa kuboresha mazingira ya hedhi safi na salama, wanaweza pia kuwawezesha wanawake na wasichana, kupunguza unyanyapaa na ubaguzi, na kuchangia katika kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu.
“Ndio maana katika maadhimisho Siku ya Hedhi Safi na Salama Duniani, ambayo huadhimishwa tarehe 28 Mei kila mwaka, GGML tuliandaa mfululizo wa shughuli za kuongeza uelewa na kutatua changamoto zinazohusiana na usafi wa hedhi.
“Mojawapo ya matukio hayo ilikuwa ni ziara ya kutembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu, ambapo wadau mbalimbali walioungana na GGML walizungumza na mamia ya wanafunzi kuhusu suala hilo muhimu,” anasema.
Anasema GGML ilimwalika mhudumu wa afya kueleza vipengele vya kibaiolojia na kisaikolojia vya hedhi na usafi sahihi wa hedhi. GGML pia ilisambaza masanduku 72 ya pedi za usafi kwa wanafunzi na kuwaonyesha jinsi ya kuzitumia ipasavyo.
Tarehe 28 Mei, GGML iliandaa mkutano wa hadhara na Halmashauri ya Mji wa Geita kuadhimisha Siku ya Usafi wa Hedhi Duniani mkoani Geita. Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali za mitaa, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wanajamii.
Anaongeza kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa ni kueneza ujumbe kwamba hedhi safi ni suala la haki za binadamu, si suala la afya tu, na kwamba kila anayepata hedhi anastahili heshima na utu.
“GGML inajivunia kuwa sehemu ya vuguvugu hili la kimataifa la kuvunja ukimya juu ya usafi wa hedhi na kuweka mazingira shirikishi zaidi na yenye msaada kwa watu wanaopata hedhi. Tunatumaini juhudi zetu zitawatia moyo wengine kujiunga nasi na kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya mamilioni ya wanawake na wasichana kote ulimwenguni,” anasema.
Akizungumzia jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na shule hiyo ya wasichana Nyankumbu, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Georgia Mugashe anasema suala la hedhi safi na salama ni kipaumbele ambacho kimewekewa mazingira salama katika kila eneo la shule hiyo.
Akianza na elimu, Mwalimu Mugashe anasema huwapa wanafunzi wa shule hiyo elimu kuhusu afya ya uzazi kila mara kwa mara na kuwafundisha namna ya kuchukua tahadhari.
“Kila mahali tumeweka pedi, mabwenini wao wanazo, kama wapo shule kuna chumba maalumu cha wasichana ambacho kimewekwa pedi na miundombinu yake.
“Nyingine zimeweka kwa daktari au nesi katika zahanati iliyopo karibu na shule hii… kwa hiyo hata kama mwanafunzi anaumwa tumbo akienda hospitali anapatiwa pedi bure kwa hiyo kila mazingira ya karibu anapewa huduma hii free,” anasema.
Anasema elimu hiyo kuhusu hedhi safi na salama inatolewa kwa ngazi zote ikianzia shuleni kwa wanafunzi kwa kushirikiana na halmashauri hata kwa wanafunzi wa shule nyingine lakini pia wanawashirikisha wazazi.
“Tunawaeleza wazazi kwamba sasa hivi suala la hedhi safi na salama ni kitu ambacho ni lazima kwa mtoto yeyote wa kike sio suala la kuficha hivyo tunazungumza nao ili nao watambue wajibu wao.
“Katika magroup ya whatsap mathalani wazazi wa wanafunzi wote wapo, hivyo tunawaeleza kabisa kwamba kila mwezi lazima atambue kuwa anatakikana kuwa na bajeti ya kumsitiri mtoto wa kike, anatakiwa kuwa na paketi moja ya pedi ambayo inauzwa Sh 1500 au 2000,” anasema.
Anasema mbali na njia hizo, pia hutumia vikao mbalimbali kuwaelekeza wazazi na watoto wa kike kuhusu umuhimu wa hedhi safi na salama ili kuzidi kuimarisha afya zao.
Pamoja na mambo mengine, Mwalimu Mkuu huyo anaishukuru Kampuni ya GGML kwa kuendeleza juhudi za kuwasaidia wanafunzi na jamii inayozunguka mgodi huo vifaa mbalimbali ikiwamo pedi ambazo zimeendelea kuwa mkombozi kwa watoto wa shule hiyo na hata kupunguza gharama za uendeshaji wa shule.
Katika maadhimisho ya siku ya hedhi duniani mwaka huu, ilikuwa na kauli mbiu ya kitaifa isemayo; “Hedhi ni tunu na Msingi wa Afya kwa wasichana na Wanawake, Tuiwezeshe,”.
Kauli mbiu hiyo ililenga kuendelea kuweka mkazo katika masuala ya hedhi iliyo salama kwa wasichana na wakina mama kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.