Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi Balozi, Eng. Aisha Amour akisisitiza jambo kwa Wahandisi Washauri akifungua Mkutano wa Mashauriano ya Wahandisi Washauri uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Eng. Bernard Kavishe akizungumza katika Mkutano wa Mashauriano ya Wahandisi Washauri uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Pichani ni Wahandisi Washauri wakifatilia hotuba ya Mgeni Rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mashauriano ya Wahandisi Washauri uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Picha ya pamoja ikimuonesha Balozi Eng. Aisha Amour (watatu kutokea kulia, mstari wa mbele) akiwa pamoja na viongozi wa Bodi ya usajili wa wahandisi katika picha ya pamoja na baadhi Wahandisi Washauri waliohudhuria Mkutano wa Mashauriano ya Wahandisi Washauri katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi Balozi, Eng. Aisha Amour akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Eng. Adv. Menye Manga (kushoto kwake) pamoja na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Eng. Bernard Kavishe (kulia kwake) akiwasili katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere tarehe 9 Juni 2023 kwenye Mkutano wa Mashauriano ya Wahandisi Washauri.
Na.Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Balozi Mhandisi Aisha Amour amezungumzia umuhimu wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini, ERB kuwawezesha wahandisi washauri wazawa ili kunufaika na kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.
Akifungua, Mkutano wa wataamu wa Wahandisi Washauri jijini Dar es Salaam leo, Balozi Amour amesema ukuaji wa uchumi unaoendelea nchini lazima uendane na ukuaji wa kada ya wahandisi washauri wazawa, na hivyo kuliwezesha Taifa kuwa na wataalamu wengi watakaofanya kazi ndani na nje ya nchi.
“Idadi ya kampuni za wahandisi washauri zaidi ya 230 na wahandisi washauri 300 haitoshi, hivyo ibueni mifumo itakayorahisisha wataalam wengi wa kihandisi kusajiliwa kuwa wahandisi washauri na kuweka madaraja mbalimbali ya kada hiyo ili kuongeza ushindani”, amesema Balozi Aisha Amour.
Katibu Mkuu huyo amesema nia ya Serikali ya Awamu ya sita ni kuhakikisha wahandisi wengi zaidi wanatumika katika miradi ya ujenzi na hivyo kunufaika na fedha nyingi zinazolipwa kwa wahandisi washauri kutoka nje ya nchi.
“Punguzeni masharti ya kusajili wahandisi washauri, hamasisheni wahandisi washauri waliopo kuomba kazi katika miradi inayoendelea, ili fedha nyingi inayoendesha miradi hiyo ibaki nchini”, amesisitiza Balozi, Eng. Aisha Amour.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, ERB, Eng. Bernard Kavishe amesema Bodi imejipanga kuhakikisha maazimio yatakayofikiwa kwenye mkutano huo yanafanyiwa kazi kwa haraka ili kuwawezesha waandisi washauri kuongezeka na kumudu ushindani kaitka soko la ndani na nje ya nchi.
“Dunia inabadilika kwa kazi hivyo na sisi wahandisi wa Tanzania tuna wajibu wa kubadilika ili kuendana na mahitaji ya dunia kwa kuhakikisha wahandisi washauri wanakuwepo na wanasajiliwa katika madaraja mbalimbali, ili kuchochea ushindani na kuleta tija kwa Taifa”, Amesema Eng. Kavishe.
Mkutano wa mashauriano wa Wahandisi Washauri ni muendelezo wa maelekezo ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ambapo aliitaka ERB kukutana na wadau ili kujadili na kupatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili Wahandisi Washauri nchini ikiwemo kuongeza idadi na kampuni za wahandisi washauri wazawa.