Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya utalii ya Camp Bastian Mikumi ,Gabriel Mwakalukwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha. Kampuni ya utalii ya Camp Bastian Co.Ltd iliyopo Mikumi inayohusika na malazi pamoja na uandaaji wa safari za wageni wa ndani na nje kutembelea vivutio vinavyopatikana Tanzania imefanikiwa kupata tuzo nane mfululizo kutokana na huduma nzuri wanazotoa kwa watalii.
Aidha katika tuzo hizo mbili zimetolewa na TANAPA huku sita zikitolewa na Trip Advisor ambapo kampuni hiyo imeshinda tuzo hizo kwa ukanda wa kusini Magharibi mwa Tanzania .
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ,Gabriel Mwakalukwa amesema kuwa,kampuni hiyo imepata tuzo hizo kwa miaka sita mfululizo kati ya Camp za watalii 60 zilizoko katika ukanda huo.
Amesema kuwa,wamekuwa wakitoa huduma nzuri kwa watalii kutokana na mafunzo bora ambayo wamekuwa wakifundisha wafanyakazi wake kuweza kuwahudumia watalii na kufurahia huduma inayotolewa na kampuni hiyo.
“Kutokana na kupata tuzo hizo tumeweza kujifunza mambo mengi sana katika kuhakikisha tunaboresha huduma zetu pamoja na kuhakikisha tunatimiza ahadi yetu ya kuwahudumia watalii ipasavyo na kuhakikisha tunaendelea kuzipambania tuzo hizo badala ya kubweteka .”amesema Mwakalukwa.
Aidha amesema kuwa kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua filamu ya Royal Tour kimeleta mafanikio na mabadiliko makubwa ikiwemo kuongeza idadi kubwa ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.
Mwakalukwa amesema kuwa,TANAPA imeangalia sana sekta ya utalii kusini kwani ilishasahaulika sana ila kwa sasa wametupia jicho kwa karibu sana hali ambayo imefanya biashara hiyo kuchangamka katika ukanda huo.
“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa namna ambayo anazidi kuipa kipaumbele sekta ya utalii hapa nchini jambo ambalo linatoa fursa kwa watalii wengi kutembelea hapa nchini na kuweza kuongeza fedha za kigeni.”amesema .