MKURUGENZI wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
Julieth Laizer ,Arusha .
Arusha.MKURUGENZI wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo,amesema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii nchini,kama kauli mbiu isemavyo” utozaji kodi kwa njia ya kiungwana kirafiki” na watazingatia maoni ya wadau wa utalii ili kuboresha huduma za kodi.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya utalii ambapo amesema mamlaka hiyo inatambua mchango mkubwa wa sekta ya utalii na wanaendelea kushirikiana nao bega kwa bega .
Amesema kuwa,utalii ukiporomoka sekta nyingine zitaporomoka, hivyo kila jambo linalohusiana na utalii litazingatiwa ili kuhakikisha sekta hiyo inatoa huduma zaidi na zilizo bora kwa maslahi ya wananchi.
“Serikali imekuwa ikisikiliza wadau wa utalii na wadau wengine lakini pia uwepo wa dawati la pamoja la utalii,hivyo sisi TRA tunazingatia hilo ili kuboresha huduma za utalii nchini na ongezeko la mapato kwa kujiepusha kuwasumbua wafanyabiashara wa utalii,”amesema.
Aidh alitoa wito kwa wananchi mbalimbali kuendelea kuunga mkono shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa kuhakikisha wanalipa kodi sambamba na kutoa na kudai risiti pindi wanapokuwa wamepata huduma yoyote.