Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) , Kanda ya Kaskazini Mhandisi Lovii Long’idu,akizungumza wakati wa semina kwa wanafunzi wa Chuo cha VETA, Babati, mkoani Manyara iliyofanyika leo Juni 5,2023.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) , Kanda ya Kaskazini Mhandisi Lovii Long’idu,akieleza majukumu ya EWURA wakati wa semina hiyo kwa wanafunzi wa Chuo cha VETA, Babati, mkoani Manyara iliyofanyika leo Juni 5,2023.
Msajili wa Wanafunzi chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi ( VETA) Bw. Sulpisi Awe,akifungua mafunzo kuhusu umuhimu wa leseni za ufungaji umeme kwa wanafunzi wa chuo hicho leo 5 Juni 2023, Babati Manyara. Mafunzo hayo yameandaliwa na EWURA Kanda ya Kaskazini inayohudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Wanafunzi wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na wataalamu kutoka EWURA Kanda ya Kaskazini leo 5 Juni 2023 Katika chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi ( VETA) Manyara
Mhandisi Tegemea Kamando akitoa mada kuhusu utaratibu wa maombi ya leseni ya EWURA ya ufungaji mifumo ya umeme leo 5 Juni 2023 VETA, Manyara.
Na.Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), leo 5 Juni 2023 imeendesha semina kwa wanafunzi wa Chuo cha VETA, Babati, mkoani Manyara kuhusu umuhimu wa leseni za ufungaji mifumo ya umeme zinazotolewa na EWURA kwa lengo la kukidhi matakwa ya usalama wa mali, maisha ya watu na utunzaji wa mazingira.
Meneja wa EWURA, Kanda ya Kaskazini Mhandisi Lovii Long’idu,amesema ushirikiano kati ya EWURA na VETA katika kutoa elimu utawafanya wanafunzi kutambua wajibu wao ulioainishwa kwenye sheria ya umeme na kanuni zake.
“Tunawaelimisha wanafunzi ili wahamasike kuomba leseni kabla ya kufanya shughuli za ufungaji umeme mitaani ili kwa pamoja tupige vita vishoka” Alieleza Mha. Long’idu.
Msajili wa Wanafunzi, VETA Manyara Bw. Sulpisi Awe, amewataka wanafunzi kutumia elimu waliyoipata katika fursa mbalimbali za kujipatia kipato mara wanapohitimu masomo yao.
Hadi sasa, mafundi umeme takribani 45 tu ndiyo waliotambuliwa kuwa na leseni katika mkoa wa Manyara huku shughuli za ufungaji umeme maeneo ya vijijini zikiongezeka, hivyo kuwepo mahitaji ya mafundi wenye weledi na sifa stahiki.
EWURA imekuwa ikifanya ukaguzi wa shughuli za mafundi umeme katika maeneo mbalimbali, na kwa mkoa wa Manyara, kuna viashiria vya kuwepo mafundi wengi wasio na leseni , hivyo mafunzo ya aina hii yatakuwa endelevu.