Na. Damian Kunambi, Njombe.
Jamii mbalimbali zimetakiwa kuenzi asili zao ikiwemo kuwekeza katika maeneo wanayotokea badala ya kujikita mijini na kuacha maeneo hayo yakiharibika na kupoteza mila na desturi zao.
Hayo ameyasema Katibu Tawala wa Wilaya ya Ludewa Daniel Ngalupela wakati akizindua kitabu cha asili ya kabila la kipangwa kijulikanacho kama Inyumba Mahame Tuvuye Khunyumba (Nyumbani kumetelekezwa turudi nyumbani) kilichoandikwa na Gastor Mtweve kwa lugha ya Kipangwa.
” Hiki kitabu kina maudhui mazuri sana! Na yenye kukuza asili zetu, zamani tulikuwa tukisimuliwa hadithi na wazee wetu na tukawa tunafurahia na kujifunza asili zetu lakini kwa sasa hivi vitu havipo jamii zetu zimejikita katika kuangalia tamthilia za mataifa mbalimbali na kusahau asili zetu”.
Naye mwandishi wa kitabu hicho Gastor Mtweve amesema ameamua kuwa balozi wa kuhamasisha watu kukumbuka asili zao na hasa wanaludewa kwa kuandika kitabu hicho ambacho kitasambazwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni ili wanafunzi waweze kujifunza mashairi mbalimbali yaliyomo katika kitabu hicho.
” Natamani sana kitabu hiki kiweze kutumika mashuleni na kuvifanyia mitiahani kama ambavyo vinavyotumika vitabu vingine vya mashairi hii itasaidia kujenga watoto wetu na kukumbuka faida za kukumbuka asili zao”.
Aidha kwa upande wa baadhi ya wahudhuliaji wa uzinduzi huo wamempongeza mwandishi wa kitabu hicho kuwa amefikiri mbali na kuwafunza kitu kizuri huku baadhi ya wahudhuliaji wa makabila tofauti na wapangwa wakionyesha matamanio ya kuandika vitabu kwa lugha zao pia.