Adeladius Makwega-MWANZA
Serikali imesema kuwa unapozungumzia maendeleo ya michezo nchini unalenga namna uwekezaji wa michezo katika nyanja mbalimbali kama vile wachezaji , waamuzi , makocha na hata madaktari wa michezo, kwa hiyo wale wanaojifunza michezo huo pia ni uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Tanzania ndugu Ali Mayay Tembele Juni 1, 2023 wakati akizungumza na wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Kwimba mkoani Mwanza waliokuwa wakifundishwa somo la Uamuzi wa Mpira wa Miguu lililokuwa likifundishwa Mkufunzi Mwandamizi Omari Mataka katika viwanja vya chuo hicho.
“Tanzania tunapata fursa mbalimbali katika michezo ulimwenguni, mathalani Ilitolewa fursa ya waamuzi wa mashindano ya Mpira wa Miguu chini ya miaka 17 kwa Afrika, malipo yalikuwa dola 4000 kuchezesha mechi moja tu, Tanzania tunao vijana wengi wenye sifa hiyo na nyinyi mbele yangu ni miongoni mwao, kwa hiyo, ninawahasisha muombe wakati wake ukifika. Kubwa kwenu muwe makini kuzingatia sheria za Mpira wa Miguu na maadili ya muamuzi.”
Wakizungumza kwa niaba ya wakurufunzi wenzao zaidi 100 wanaosoma somo hilo , mwanachuo Ezra Lupoli amesema kuwa anamshukuru sana Mkurugenzi wa Maendeleo kwa kufika katika chuoni hapo, hiyo ni fursa kubwa sana kwao huko akisema kuwa mkufunzi Omari Mataka anawafundisha vizuri somo lake.
“Kati ya wakurufunzi wenzangu hawa, wapo wanaochezesha mpira wa miguu katika ngazi mbalimbali na darasa hili mbele yako tunakuhakishia tutafanya vizuri mno katika uamuzi wa mpira wa miguu kwa wanaume na wanaweake, mbele yako tunaomba seti kumi za bandera za waamuzi.”
Kwa upande wake Ruaida Hassan mwanachuo wa kozi ya ngazi ya Cheti cha Elimu Kwa Michezo anayetokea Wilaya ya Magharibi A mkoa wa Mjini huko Zanzibar amesema anaufahamu utendaji kazi ya mkurugenzi Mayay kwani anakutana naye katika vikao kadhaa vya michezo huku akisema,
“Nawaomba wanawake wenzangu washiriki katika michezo maana fursa zipo nyingi na ndiyo maana nimefunga safari ndefu kutoka Zanzibar na kufika Malya kusoma mafunzo haya.”
Mkurugenzi Ali Mayay mwishoni aliwahakishia wanachuo hao kuwapatia seti kumi za bendera za waamuzi wa soka akisema wazi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa kila Mtanzania anayetumia muda wake kushiriki michezo na hiyo sera ya Serikali aya Awamu ya Sita ya inayoongozwa mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.