Na. Gideon Gregory, Dodoma.
JESHI la Kujenga taifa (JKT), limekanusha uzushi unaotolewa katika mitandao ya kijamii ya kuwa katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa kuna unyanyasaji wa kijinsia kwa vijana wanaoripoti kwa ajili ya mafunzo ya kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 2,2023 katika Makao Makuu ya JKT Mkoani Dodoma ,Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema,JKT kwa kushirikiana na mamlaka nyingine watachukua hatua kwa waliohusika kutokana na kulichafua Jeshi hilo.
“Kumekuwa na uvumi wa namna hii kila mwaka tunapoita vijana hasa wa mujibu wa sheria unaoashiria JKT kuna manyanyaso,hii siyo kweli taarifa hizo zipuuzwe
JKT limekuwa likichukua vijana wa mujibu wa sheria kila mwaka na wale wa kujitolea kwa lengo la kuwapa vijana mafunzo yaliyoandaliwa ili kuwajenga uzalendo,ukakamavu na kuwajengea ari ya kulilinda Taifa lao kwa nguvu zao zote .”
Amesema,JKT ndiyo sehemu salama ya kuwafanya vijana wafuate utamaduni wao badala ya kufuata tamaduni za nchi nyingine kupitia utandawazi.
Aidha amesema kuwa katika kuhakikisha mafunzo hayo yanawafikia walengwa JKT limeweka utaratibu mzuri na kila kamba linamlezi mwanamke (Matron) na mlezi mwanaume (Patron) ambao wanakuwa nao karibu wawapo kambini.
Ameongeza kuwa “Na endapo ikabainika kuna mkufunzi anakwenda kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa za miongozo ya malezi ya vijana ndani ya JKT hatua kali za kinidhamu na kisheria zinachukuliwa dhidi yake” amesema.
JKT imetoa rai kwa umma wa watanzania kuwa mtu yeyote mwenye nia ovu ya kueneza taarifa za uzushi na uongo zinazohusu JKT katika mitandao ya kijamii atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataka vijana wote walioitwa kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2023 kuripoti katika makambi waliyopangiwa tayari kuanza mafunzo