Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (kushoto) akimnyoshea kidole Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Gabriel Mayaya (kulia) wakati akimsisitizia kukamilisha ujenzi wa miradi haraka iwezekanavyo kabla ya Julai 1, 2023 wakati wa ziara yake ya kuhimiza ukamilishaji wa miradi hiyo aliyoifanya leo Juni 1, 2023 wilayani humo.
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amemtaka Mhandisi na Afisa
Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuhakikisha wanakamilisha ujenzi
wa wodi ya wanaume na wanawake pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti (Mochwari)
katika Hospitali ya Wilaya hiyo kabla ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya kazi
hiyo kurudishwa Hazina.
Serukamba ametoa agizo hilo leo (Juni 1, 2023) katika mfululizo wa ziara
yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni
kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha
wa 2022/ 2023 ambapo zimebaki siku 19 kuisha.
Maofisa waliokali kuti kavu ni Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Gabriel Mayaya ambaye alielezwa kuwa
kama fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo zilizoletwa kwenye wilaya hiyo
zitarudishwa Hazina kutokana na kutokamilika kwa miradi hiyo kabla ya Juni 30,
mwaka huu awe na uhakika kuwa atakuwa hana kazi.
“Mhandisi hakikisha unakamilisha ujenzi wa miradi yote kwa wakati na
kama fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitarudishwa
Hazina bila ya kukamilisha kazi hii utakosa kazi,” alisema Serukamba kwa
ukali.
Kwa upande wa Afisa Manunuzi, Joseph
Nswila alielezwa kuwa iwapo kesho (Ijumaa) atashindwa kupeleka mabati ya
kuezekea chumba cha kuhifadhia maiti atamuweka ndani.
Serukamba alikerwa na kasi ndogo ya ukamilishaji wa miradi ya maendeleo
inayotekelezwa katika wilaya hiyo kutokana na uzembe unaofanywa na viongozi kwa
kushidwa kusimamia na badala yake wamewachia viongozi wa vijiji,kata na kamati
za ujenzi jukumu la kusimamia.
Mkuu wa Mkoa alisema serikali
imeleta fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi ya
maendeleo hivyo ni lazima wakuu wa idara wagawane kuisimamia ili iweze
kukamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu.
Alisema itakuwa jambo la ajabu kama fedha hizo ambazo zimeletwa katika mkoa
huu zitarudishwa Hazina kutokana na kutokamilika miradi na kwamba hali hiyo
ikitokea maana yake viongozi watakuwa wamefeli na kushindwa kumsaidia Rais
Samia Suluhu Hassani ambaye amehangaika kuzitafuta fedha hizo.
Miongoni mwa maafisa waliopata fursa ya kutembelea na kukagua miradi hiyo
ni wataalam, watendaji wa kata, tarafa, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama
wa wilaya hiyo na viongozi wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania
(SMAUJATA) wilayani humo ambao ni Wales Shechambo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa
wa Mwembeni, Salutary Naaly na Hossen Kheri.
Miradi aliyoitembelea na kuikagua ni ujenzi wa wodi ya wanaume, wanawake na
chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, kutembelea
stendi ya mabasi na eneo itakapojengwa stendi mpya, ujenzi wa madarasa Shule ya
Msingi Tambukareli, ujenzi wa Zahanati
ya Kijiji cha Mbwasa, Ujenzi wa Bweni la Wasichana Shule ya Sekondari ya
Sasajila mradi ambao umefadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na ujenzi
wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kintinku na ujenzi wa
madarasa katika Shule ya Msingi Chikuyu.
Kesho ziara hiyo itaendelea wilayani humo kwa kukagua miradi mbalimbali na
kuwahimiza wahusika kuikamilisha kwa wakati.