Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akizungumza na wananchi wa vijiji vya Chikomo na Chinunje wilayani humo wakati wa kampeni za uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo iliyofanyika jana.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
JAMII imetakiwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali katika kampeni za kuwaibua watu walio ambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu ili waweze kuanzishiwa matibabu badala ya kuwaficha majumbani.
Wito huo umetolewa na mratibu wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole, wakati wa kampeni ya uelimishaji,uibuaji na uchunguzi wa ugonjwa wa Tb iliyofanyika katika kijiji cha Chikomo Chinunje kata ya Mbesa wilayani humo.
Dkt Kihongole alisema, licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kutokomeza ugonjwa huo,hata hivyo changamoto kubwa ni ushiriki mdogo wa jamii katika kutokomeza ugonjwa huo unaoendelea kupoteza maisha ya watu wengi hapa nchini.
Alisema,ugonjwa huo bado ni tatizo kubwa katika wilaya ya Tunduru kutokana na muingiliano na baadhi ya nchi jirani,kwa hiyo zinahitajika nguvu za pamoja kati ya Serikali,viongozi wa kisiasa na jamii nzima.
Alisema ili kutokomeza kabisa ugonjwa huo wilayani Tunduru,umoja na ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2033 ambapo amewapongeza wadau Shirika la Amref Healt Africa na MDH kwa kushiriki katika kampeni za kupambana na TB wilayani humo.
Alisema,ugonjwa wa kifua kikuu unatibika kwa mgonjwa kuwahi Hospitali na kupata tiba sahihi na kuwataka wananchi kuachana potofu kwamba ugonjwa huo hauna dawa.
Alisema,wamelazimika kurudi kwa ajili ya kufanya kampeni kwa mara ya pili katika vijiji hivyo kwa sababu hali ya maambukizi ya kifua kikuu bado ni tishio kutokana na umbali hadi kufika katika vituo vya kutolea huduma za matibabu zinazopatikana Hospitali ya Mbesa na Hospitali ya wilaya Tunduru mjini.
Aidha,amevishukuru vyombo vya Habari vya ITV na Magazeti ya Serikali Habarileo na Dailynews kwa mchango wa kuelimisha jamii kuhusiana na madhara ya ugonjwa huo,hali iliyosaidia wananchi wengi kufikiwa na elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.
Amewaomba wananchi,kutoa ushirikiano kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii waliopo katika maeneo yao wanaofanya kazi ya kukusanya makohozi na kupeleka Hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
Said Mohamed mkazi wa kijiji cha Chikomo,ameiomba Serikali kupitia wizara ya afya kuendelea kufanya kampeni za kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu ili kuwasaidia walioambukizwa na ugonjwa huo waweze kupata matibabu.
Alisema,katika kijiji hicho kuna watu wanaugua Tb,lakini bado hawajapa matibabu kutokana na umbali uliopo hadi kufika kwenye vituo vya huduma na wako majumbani,lakini kama wangepatiwa tiba sahihi wangeweza kupona na kupata nafasi ya kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Chinunje Bakari Chakupewa,ameipongeza Hospitali ya wilaya Tunduru kuendelea na kampeni hizo kwani zimesaidia sana kuokoa maisha ya watu wengi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini.