Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Mwembeni wilayani Manyoni na Viongozi wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wilayani humo wakiwa kwenye kikao cha kupanga mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kilichofanyika jana May 29, 2023.
………………………………………..
Na Dotto Mwaibale, Manyoni.
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi
la Mwembeni Wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwa kushirikiana na Shujaa wa
Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA
wamekutana katika kikao kazi cha kuweka mikakati kabambe ya kutokomeza
vitendo vyote vya ukatili wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa
SMAUJATA Wilaya ya Manyoni Shujaa Napegwa Jared alisema kikao hicho ni cha
muhimu sana katika kutokomeza ukati katika wilaya hiyo hasa kitongoji cha
Mwembeni.
“Tumekutana leo na wenzetu wa Kamati ya
Siasa ya CCM wa kitongoji cha Mwembeni kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya
kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani kwetu pamoja na eneo la
Mwembeni ambalo lina watu wengi kutokana na kuwa ndani ya mji wa Manyoni na
kuwepo kwa vitendo hivyo,” alisema Jared.
Alisema CCM inanafasi kubwa katika kusimamia
mmomonyoko wa maadili ya jamii ukiwemo ukatili wa kijinsia ndio maana
wakaona ni vema wakae pamoja kwa lengo la kuongeza nguvu ya kukabiliana na
jambo hilo ambalo limeonekana kukithiri maeneo mengi hapa nchini hususani katika wilaya hiyo.
Alisema wilaya ya Manyoni ni kongwe na
inamwingiliano wa watu wengi kutoka sehemu mbalimbali jambo ambalo
limechangia kuwepo na vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kitongoji cha
Mwembeni, Salutary Naaly, alisema kikao hicho cha pamoja SMAUJATA na Kamati ya
Siasa ya CCM ya eneo hilo kitaleta tija kubwa katika mapambano ya kutokomeza ukatili
wa aina yoyote ile kwenye wilaya hiyo na kitongoji hicho.
“Kitongoji chetu hiki kimekuwa na
muingiliano wa watu wengi na kusababisha kuwepo kwa ukatili wa kijinsia, kupitia ushirikiano huu tutapiga hatua kubwa kukabiliana na vitendo
hivyo kwani umoja ni nguvu,” alisema Naaly.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Tawi la
Mwembeni, Joseph Sajilo alisema kupitia
umoja na ushirikiano huo hakuna jambo litakalo shindikana katika
kukabiliana na kutokomeza vitendo hivyo wilayani humo hasa katika kitongoji
hicho.
“CCM ni Chama kikubwa na ndicho kimekamata
dola hivyo napenda kuwaambia kuwa kwa ushirikiano huu hatutashindwa kutokomeza
ukatili katika wilaya yetu na hapa Mwembeni,” alisema Sajilo.
Katika kikao hicho ajenda kubwa ilikuwa ili
kutokomeza vitendo hivyo ni kudumisha
ushirikiano, umoja na upendo baina ya wananchi, SMAUJATA, CCM na vyombo vya dola.