Na Mwandishi wetu, Mirerani
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Manyara Karoline Albert Mthapuka amefungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo maafisa utumishi wa Mkoa huo, makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na maafisa utumishi wa Halmashauri saba za Wilaya za mkoa huo kwenye ukumbi wa Mazubu Grand Hotel Mji mdogo wa Mirerani.
RAS Mthapula akizungumza wakati akifungua kikao kazi hicho amesema watumishi hao wana dhamana kubwa ya kufanikisha utendaji kazi wao kwa kutoa huduma bora.
Amesema watumishi wenzao wakifika katika ofisi zao wawasikilize kwa makini na kuhakikisha wanasuluhusha changamoto zao kwa muda muafaka.
Amesema wanapaswa kuvaa viatu vya wote wanaofika kwenye ofisi zao ili watatuliwe changamoto zao na kuweza kupatikana kwa ufanisi makazini mwao.
“Tuzingatie maadili, utaratibu wa kushughulikia uhamisho wa watumishi wa mamlaka za Serikali za mitaa na utekelezaji wa muundo mpya wa mamlaka za Serikali za mitaa,” amesema RAS Mthapula.
Katibu Tawala Msaidizi utawala na rasilimali watu, Dominick Mbwette amesema mafunzo hayo ya siku mbili yatawajengea uwezo zaidi washiriki hao katika kutimiza majukumu yao makazini mwao.
Mbwette amesema wawezeshaji wa mafunzo hayo ni maofisa kutoka ofisi ya Rais utumishi na TAMISEMI.