Mwezeshaji katika Mdahalo wa kupinga Ukatili wa KijinsiaJackson Malangalila kutoka Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) akizungumza na wanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari Lunguya hawapo pichani
Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Lunguya wakiandika ujumbe wa kupinga ukatili kwenye Bango wakati wa Mdahalo wa kupinga ukatili
Mwanafunzi kidato cha Tatu katika shule ya sekondari Lunguya Lameck John akichangia Mada kwenye mdahalo wa kupinga ukatili wa kijinsia
Na Salvatory Ntandu – Msalala
Uanzishwaji wa midahalo ya kupinga ukatili wa kijinsia katika Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kupitia mradi wa Ushirikishwaji wa Jamii kwa njia ya Midahalo wenye dhima ya kutokomeza ukatili na mila na desturi hasi kwenye jamii imetajwa kuleta tija kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuzitambua haki zao za msingi.
Hayo yamebainishwa leo na baadhi ya washiriki wa Mdahalo huo akiwemo Godfrey Tinya, Mwanafunzi wa Darasa la sita Shule ya Msingi Lunguya wakati akichangia hoja hiyo amesema ipo haja ya kuundwa kwa klabu za kupinga ukatili zitakazowawezesha kupaza sauti uliofanyika katika shule ya Msingi Lunguya.
Amesema kuwa wapo baadhi ya wanafunzi pindi wanapofika darasa la Saba hushawishiwa na wazazi wao wafanye vibaya katika mtihani wa mwisho ili wakaozeshwe,au kuozeshwa hali ambayo husababisha kukosa haki zao za msingi za kielimu na endapo Klabu zitakuwepo zitasaidia kuibua ukatili huo.
Naye Patrick Magembe Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Lunguya amesema Klabu hizo zitasaidia kukemea vitendo vya ukatili kwa wanafunzi wa kike katika jamii kwani wengi wao watakuwa wanazitambua haki zao za msingi.
“Midahalo hii ina tija tunaomba Serikali na Wadau tuendelee kujengewa uwezo pindi zitakazoanzishwa Klabu hizi zitasaidia kuleta matokeo chanya kwetu na ni msaada kwa wanafunzi wa kike ambao hawana sehemu pa kupazia sauti,”amesema Magembe.
Kwa upande wake Tumain Makemba mwalimu wa Malezi katika shule ya sekondari Lunguya amesema kuwa watahakikisha wanasimamia zoezi la uanzishwaji wa klabu hizo na kutoa rai kwa serikali na wadau wengine kuzijengea uwezo pindi zitakapoanzishwa ili ziweze kuwa na uwezo wa kujiendesha.
Akizungumza katika Mdahalo huo Jackson Malangalila kutoka Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Wakuu wa Shule hizo wanaweza kuanzisha Klabu hizo ili kuleta matokeo Chanya kutokana na mradi huo kujumuisha makundi mbalimbali katika jamii ili kuwa sehemu ya kupaza sauti kwa wenzao wenye jinsi ya Kike.
“Mradi huu unatekelezwa kwa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) na Shirika la Misaada la Korea Kusini (KOICA) ,”amesema Malangalila.
Amefafanua kuwa TGNP inasimamia uendeshaji wa midahalo hiyo ili kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule za Msingi na sekondari kuhusiana na namna bora ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii ambavyo havijaripotiwa ili mamlaka zinazohusika ziwezekuchukua hatua.
Kwa mujibu wa Takwimu za hali ya ukatili nchini zilizotolewa jana Katika Halmashauri ya Msalala na Kamishina wa Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile amesema idadi ya Matukio ya ukatili yameongezeka na kufikia 30,566 kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na matukio 1193 kwa mwaka 2021.
Amesema mwaka 2022 matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa 12163 ikilinganishwa na matukio 11419 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la matukio 670.