Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
mkoani Singida, Ally Mwanga (katikati) akiongoza kikao cha kawaida cha baraza
la madiwani cha robo ya tatu kuanzia Januari hadi Machi 2023 kilichoketi
wilayani humo May 19, 2023.Kushoto ni Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovson Mtangeki na kulia ni Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo, Justice Kijazi.
Na Dotto Mwaibale, Ikungi
ONGEZEKO kubwa la vijana
kushiriki michezo ya kubashiri (Kubeti), limedaiwa kusababisha ndoa kuvunjika
na kukithiri kwa uhalifu katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Mtunduru,
Ramadhan Mpaki wakati akichangia kwenye kamati ya fedha na uchumi katika kikao
cha baraza la madiwani cha robo tatu kuanzia Januari hadi Machi 2023 kilichoketi
May 19, 2023 wilayani humo.
Mpaki alisema kwa siku za karibuni kumekuwa na
kasi kubwa ya ndoa kuvunjika na uhalifu kuongezeka na sababu kubwa ni kutokana
na vijana kujihusisha na michezo ya kubashiri.
Diwani huyo alisema iwapo hakutakuwa na hatua za
haraka kudhibiti michezo ya kubashiri ni wazi kuwa hali itazidi kuwa mbaya, kwa
ndoa kuvunjika na uhalifu kuongezeka.
Mpaki alitoa ushauri kwa baraza la madiwani
kuangalia namna ambayo inaweza kufikisha jambo hili katika mamlaka za kutunga sheria ili ziweze kuona
namna ya kulitatua, kwani hali ni mbaya kwa sasa hasa kwa wanandoa.
“Naomba halmashauri yetu iangalie upya sheria ya mchezo
huu wa kubashiri, kwani pamoja na kuwa chanzo cha mapato vijana wamekuwa
wakicheza mchezo huo hadi usiku wa manane ambapo pia wamekuwa wakipanga vitendo
vya kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na kutishia ndoa za watu,” alisema Mpaki
bila ya kufafanua.
Aidha diwani huyo aliwataka watendaji wa
halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukasanyaji wa mapato, huku wakizingatia
misingi ya utawala bora.
Naye Diwani wa Kata ya Mwaru, Iddi Makangale
alimpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ally Mwanga na Mkurugenzi, Justice Kijazi kwa mafanikio
makubwa inayopata wilaya hiyo chini ya uongozi wao kwa kushirikiana vizuri na
watendaji wa kata, tarafa na wataalam.
Pia Makangale alizipongeza kata za Mgungila, Mwaru
na Mkiwa kwa kuongoza kwa kukusanya mapato na kuzitaka kata zingine kuiga mfano huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ally Mwanga
aliwataka watumishi wote na viongozi kuwa wazalendo na kushirikiana ili kuiletea
maendeleo wilaya hiyo.
Mwanga alisema suala la ukusanyaji wa mapato ni
la kufa na kupona na akasisitiza uzalendo katika jambo hilo na kuwa uhai wa
halmashauri yoyote unatokana na mapato na si vinginevyo.
Awali Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovson
Mtangeki, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson aliipongeza
halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa miaka tisa mfululizo na kuwa
mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa kada zote za utumishi wakiwamo
madiwani na Serikali.
Alisema halmashauri hiyo imekuwa na miradi
mbalimbali ambayo inatekelezwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha na
kuwa kazi ya ukaguzi ni lazima ifanywe na viongozi wote na si kumuachia mkuu wa
wilaya peke yake.
Alisema licha ya kuwepo kwa kamati, wataalam,
maafisa kata na tarafa kwa ajili ya kusimamia miradi hiyo katika utekelezaji wake
madiwani hawawezi kukwepwa kwa namna yoyote ile ukizingatia kuwa miradi mingi
inayofanyika ipo kwenye maeneo yao.
“Mheshimiwa Mwenyekiti nimesimama mbele ya baraza
lako hili tukufu kuwaomba madiwani wetu walau wawe wanakwenda kuikagua miradi
hiyo mara mbili kwa wiki watakuwa wamesaidia kwani nguvu yao inahitajika sana,”
alisema Mtangeki.
Aliwaomba madiwani hao kuilinda,kuisimamia na
kuwahamasisha wananchi waweze kushiriki katika utekelezaji wake na itekelezwe
kwa wakati na viwango vinavyohitajika.
Katika hatua nyingine Mtangeki aliomba wakati wa
utekelezaji wa miradi hiyo vitu vinavyosaidia ujenzi kama mchanga, mawe na vingine
vifikishwe eneo la ujenzi siku moja kabla tofauti na ilivyo sasa ambapo huwa
vinapelekwa siku ya kazi jambo ambalo linawafanya mafundi wasifanye kazi kwa ufanisi.
Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Justice Kijazi alisema mwaka wa fedha
wa 2023/ 2024 madiwani wote wa halmashauri hiyo watafanya ziara ya mafunzo
kwenda Wilaya ya Tanganyika kujifunza namna bora ya utunzaji wa mazingira
kutokana na wilaya hiyo kuwa kinara wa utunzaji mazingira hapa nchini.
Hatua hiyo ilifikiwa na Kijazi kufuatia maombi ya
baadhi ya madiwani kuomba kufanyika kwa ziara hiyo ambayo itakuwa na tija kwa
halmashauri hiyo kwenye suala zima la uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Katika kikao hicho watumishi wa halmashauri hiyo
walioongoza kwa ukusanyaji wa mapato akiwepo mratibu wa nyumba za halmashauri
hiyo zilizopo Manispaa ya Singida, Jonath Lutiga walipatiwa zawadi ya fedha
taslimu kuanzia Sh. 300,000 kama motisha ili kuwafanya kuwa na mori wa
kuendelea kufanya kazi kwa bidii.